Arusha. Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam imewaachia huru washtakiwa wawili, akiwemo Ofisa wa zamani wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Ngamba Mtopa, waliokuwa wakishtakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi kilo 168.49.
Ngamba alikuwa na nambari za kijeshi MT 71478, kutoka Kongowe, jijini Dar es Salaam na mwenzake Silvanus Sebastian.
Hukumu hiyo ilitolewa Ijumaa, Julai 25, 2025, na Jaji Sedekia Kisanya, aliyesema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha pasipo kuacha shaka shtaka dhidi yao.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa Desemba 22, 2023, katika eneo la Mwembe Mohoro, Ikwiriri, wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani, washtakiwa walikutwa wakisafirisha dawa hizo kinyume cha sheria.
Walidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na Kifungu cha 15(1)(a) na (3)(iii) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Sura ya 95, kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2019, na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Kifungu hicho kilisomwa pamoja na aya ya 23 ya Jedwali la Kwanza la sheria hiyo na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Kudhibiti Uhalifu wa Kiuchumi na Kuratibu (EOCCA).
Ili kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba ambao ni Ermest Prosper, F7331 Sajenti Yohana kutoka Kituo cha Polisi Ikwiriri, G9704 Koplo Paschal, H9570 Koplo Shaban, PF20950 Inspekta Raphael Shimenyi, Hassan Sospeter, na G8781 Koplo William.
Mbali na mashahidi hao, upande wa Jamhuri ulikuwa na vielelezo 12, ikiwemo mifuko tisa yenye bangi, sare moja ya kijeshi na cap (J219t), kitambulisho cha jeshi chenye jina la MT 71478 Ngamba, na gari aina ya Toyota Gaia lililokuwa na namba za usajili T 708 BQR.
Ilidaiwa kuwa usiku wa tukio, shahidi wa tano akiwa kazini alipokea taarifa za kiintelijensia kutoka kwa mtoa taarifa, akihusisha gari hilo na mchakato wa kusafirisha dawa hizo.
Ilielezwa kuwa aliwajulisha wakuu wake na kupata amri ya upekuzi (kielelezo cha 10), akapanga timu ya maofisa na kuelekea eneo la tukio walipojipanga kulinasa gari hilo.
Ilielezwa gari hilo lilisimamishwa na shahidi wa tano, aliyejitambulisha kwa washtakiwa na kuwaeleza kuwa wanashukiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya. Upekuzi ulifanywa mbele ya shahidi wa tano na wa sita, na kubaini mifuko tisa iliyosadikiwa kuwa bangi.
Mbali na mifuko hiyo, vitu vingine walivyokutwa navyo ni simu mbili, sare ya jeshi, kofia na kitambulisho cha jeshi. Mashahidi hao wawili, pamoja na washtakiwa, walisaini hati ya ukamataji.
Shahidi wa tano alieleza kuwa baada ya kukamata vitu hivyo, vilipelekwa Kituo cha Polisi Ikwiriri na kukabidhiwa kwa shahidi wa nne, ambaye alifungua jalada la kesi IKW/IR/1471/2023.
Shahidi wa pili alithibitisha kuandika kwenye daftari la vielelezo, na Desemba 27, 2023, mifuko hiyo tisa ilikabidhiwa kwa shahidi wa tatu kwa ajili ya kuwasilishwa kwa Mkemia wa Serikali wa Mamlaka ya Maabara ya Dar es Salaam.
Shahidi wa kwanza, ambaye ni Mkemia kutoka GCLA, alikiri kupokea mifuko hiyo na kuchunguza majani yaliyokuwemo ndani. Baada ya kuyapima, iligundulika kuwa ni bangi yenye uzito wa kilo 168.49.
Katika utetezi wao, mshtakiwa wa kwanza alidai kuwa siku ya tukio alikuwa safarini kuelekea Rufiji kushiriki kikao cha familia kuhusu mirathi ya baba yake aliyefariki.
Alieleza kuwa akiwa stendi ya mabasi ya Ikwiriri akisubiri usafiri wa kwenda kijijini kwao, alifikiwa na kuhojiwa na askari polisi, na licha ya kujitambulisha, alikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Ikwiriri.
Alidai kuchukuliwa vitu vyake binafsi, ikiwemo kitambulisho cha kazi, fedha taslimu Sh76,000, mkanda, na alikaa mahabusu kwa siku saba kabla ya kufikishwa mahakamani. Kwa mara ya kwanza alifahamu shtaka akiwa mahakamani.
Aidha, alivikana vielelezo vyote vinavyohusiana na kosa hilo, yakiwemo magunia tisa ya bangi, kofia ya kijeshi, simu, na kitambulisho chake cha kazi ambacho alisema kilichukuliwa na Polisi.
Alikanusha kuwa alikamatwa kwenye gari, hakuwahi kuwa na gari hilo, alikana saini yake na alama ya kidole gumba, na alisisitiza kuwa hakuwahi kusaini popote.
Mshtakiwa wa pili alidai kuwa ni mfanyabiashara wa mbuzi aliyesafiri hadi Ikwiriri kwenda kwenye mnada uliopangwa kufanyika siku iliyofuata.
Baada ya kutumia siku nzima kutafuta mbuzi na makazi, alikamatwa usiku na askari waliodai alikuwa akirandaranda.
Alidai kuwa alikaa mahabusu kwa takribani wiki moja kabla ya kufikishwa mahakamani. Hakujulishwa sababu za kukamatwa hadi alipofunguliwa shtaka.
Alikanusha kumfahamu mshtakiwa wa kwanza, gari hilo, magunia tisa ya bangi yaliyotolewa mahakamani, simu wala kuandika maelezo ya onyo.
Jaji Kisanya alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote, suala kuu ni iwapo upande wa mashtaka umethibitisha kosa la kusafirisha dawa za kulevya bila shaka yoyote, kwa mujibu wa sheria.
Alisema upande wa Jamhuri ulitegemea ushahidi wa shahidi wa tano na sita, hati ya upekuzi, cheti cha ukamataji kilichodaiwa kusainiwa kwa alama za dole gumba na washtakiwa.
Hata hivyo, baada ya kupima ushahidi kwenye rekodi, Jaji hakuridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha pasi shaka kuwa magunia hayo ya bangi (kielelezo cha nne) yalikamatwa kutoka kwa washtakiwa.
“Shahidi wa sita, ambaye alikuwa shahidi wa kujitegemea, awali alidai kuwa anaweza kuwatambua watu waliokutwa na mifuko hiyo, lakini alishindwa kuwatambua mahakamani,” alisema.
Jaji alisema kutofanyika kwa uchunguzi zaidi juu ya sababu ya kushindwa kwa shahidi huyo kuwatambua washtakiwa kunatia shaka.
Aliongeza kuwa ushahidi mwingine wa maungamo ya mdomo yaliyodaiwa kutolewa mbele ya mashahidi, haukuwasilishwa mahakamani kama ushahidi wa maandishi wala kufuata utaratibu wa kisheria.
“Kwa hiyo, kwa kukosekana kwa taarifa zilizoandikwa na bila ushahidi wa kufuata utaratibu, maungamo ya mdomo hayawezi kuwa ushahidi wa kuaminika,” alisema.
Jaji huyo alihitimisha kuwa upande wa mashtaka haukufikia viwango vya kisheria kuthibitisha kuwa magunia hayo tisa ya bangi yalikamatwa kwa washtakiwa, na kwamba upekuzi na ukamataji ulizingatia sheria.
Baada ya kuchambua hoja zote, Jaji Kisanya alisema Mahakama inawaachia huru washtakiwa waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kusafirisha dawa za kulevya, na kuagiza mifuko hiyo iharibiwe kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu gari, simu mbili, sare za kijeshi na kofia ya kijeshi zilizokataliwa na washtakiwa wote wawili, Jaji aliagiza virejeshwe kwa Jeshi la Polisi Tanzania, huku kitambulisho chenye jina la MT 71478 Ngamba kikitakiwa kurejeshwa kwa mshtakiwa wa kwanza.