UONGOZI wa Simba unaendelea kuboresha kikosi chake kinachonolewa na Fadlu Davids ukisaka mastaa kutoka ndani na nje ya nchi, huku ukiwa tayari umeshamalizana na nyota kadhaa wanaotarajiwa kuonekana katika mitaa ya Msimbazi msimu ujao wa mashindano.
Inaelezwa kwamba lile fuko la fedha ambalo bilionea wa timu hiyo Mo Dewji aliahidi hivi karibuni kwamba ataliachia ili kufanyia usajili limefanikiwa kuwanasa mastaa wawili ambao msimu uliomalizika wa Ligi Kuu Bara walikipiga na kuvuja jasho kwelikweli.
Taarifa ilizonazo Mwanaspoti zinaeleza kwamba wachezaji hao ni ni beki wa kushoto Miraji Abdallah ‘Zambo Junior’ na kiungo mkabaji Charles Semfuko ambao wote walikuwa wakikipiga Coastal Union ya Tanga na tayari mmoja inaelezwa kwamba ameshatua jijini Dar akijiandaa kwa safari ya kwenda Misri ambako mwisho wa mwezi huu chama hilo linakwenda kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya.
Alikuwa na wakati mzuri msimu uliopita akicheza zaidi ya mechi 20 Coastal Union na inaelezwa amesaini mkataba wa miaka mitatu kuitumikia Simba akiongeza nguvu upande aliokuwa anacheza nahodha wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Tshabalala aliyehudumu Simba kwa misimu 11, ametimka kikosini humo na sasa uongozi unapambana kupata mbadala sahihi ukinasa saini ya mchezaji huyo ambaye yupo kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kinachojiandaa na CHAN 2024.
“Ni kweli tumemalizana na beki huyo, matarajio ni makubwa kwake, tunategemea atakuwa mchezaji sahihi na tumempata kwa wakati sahihi kucheza kikosini kwetu,” kilisema chanzo kutoka Simba.
“Pia tuna mpango wa kuongeza nguvu kwa kusajili mchezaji mmoja upande huo aliokuwa anacheza Tshabalala.”
Mwanaspoti linafahamu Simba ilikuwa kwenye mazungumzo na beki wa Al Hilal ya Sudan, Khadim Diaw, raia wa Senegal ili kuongeza nguvu katika beki ya kushoto baada ya kuondoka kwa Tshabalala aliyemaliza mkataba na Valentin Nouma ambaye alifikia makubaliano ya kusitisha mkataba.
Simba pia inadaiwa kufanya mazungumzo na beki mwingine wa kushoto kutoka JKT Tanzania, ambaye ni mzawa Karim Bakari Mfaume.
Simba inadaiwa kumalizana na Semfuko kwa kumpa mkataba wa miaka mitatu ambapo nyota huyo ni zao la Coastal Union akianzia timu ya vijana kabla ya kupandishwa kikosi cha timu kubwa.
Taarifa zinabainisha kiungo huyo tayari amemalizana na Simba na jana Jumamosi amejiunga na kikosi tayari kwa maandalizi ya msimu mpya.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Coastal Union kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli wamekaa mezani na Simba na kufanikiwa kufanya biashara ya kumuuza mchezaji huyo.
“Ni kweli tumefanya biashara ya kumuuza Semfuko ambaye anaenda kuitumikia Simba msimu ujao baada ya makubaliano ya pande zote mbili tunamtakia kila lakheri kwenye majukumu yake mapya,” kilisema chanzo.
“Mpira ni biashara hatukuwa na sababu ya kumzuia mchezaji kwenda kujaribu maisha mengine nje ya Coastal Union tunaamini ataenda kufanya vizuri akipewa nafasi ya kucheza ni kipaji kizuri sana na ana nidhamu ya mpira.”
Chanzo hicho kilisema Simba ni timu ambayo imekuwa ikifanya biashara nzuri na Coastal kwani sio mchezaji wa kwanza kuwauzia kikimtaja beki Ame Ally ambaye sasa ametimkia Mbeya City na Victor Akpan.
Kwa upande wa Simba chanzo kimedai kuwa imemnasa mchezaji huyo kwa mkataba wa miaka mitatu.
“Tumemalizana na Semfuko kwa kumsainisha mkataba wa miaka mitatu. Ni pendekezo la kocha na kuhusu mkataba wa muda mrefu inatokana na umri wake lakini pia ni mchezaji ambaye tunaamini atakuja kuwa degemeo la kikosi cha timu ya taifa miaka ijayo,” kilisema chanzo hicho.
Semfuko anakwenda kuungana na Yusufu Kagoma kwenye nafasi ya kiungo mkabaji wakiwa wachezaji wazawa. Mzawa mwingine ni Mzamiru Yassin ambaye mkataba wake umemalizika lakini bado haijawekwa wazi hatima yake. Katika eneo hilo, Simba tayari imetangaza kuachana na viungo watatu wa kimataifa Fabrice Ngoma, Augustine Okejepha na Debora Mavambo.