Masista waliofariki kwa ajali Moshi, Kanisa Katoliki latoa pole

Moshi. Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro likiendelea kumshikilia Saimon Paul, dereva aliyesababisha ajali iliyoua masista (watawa) wawili wa Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi, kanisa hilo kupitia mashirika ya masista hao, limetoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao.

Masista hao, ambao wanatoka mashirika tofauti ya kitume katika jimbo hilo, walifariki dunia Julai 25, 2025 katika eneo la Bomang’ombe, Wilaya ya Hai, wakati wakitoka kwenye sherehe, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuligonga gari jingine kwa nyuma na kusababisha vifo vyao, huku wengine 11 wakijeruhiwa.

Waliofariki katika ajali hiyo ni Sista Agatha Shirima (24) wa Shirika la Masista la Veronica wa Uso Mtakatifu wa Yesu na Sista Calista Mtenga (76) wa Shirika la Masista la Wafransiskani Wakapuchini wa Maua.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Julai 26, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva ambaye alikuwa akiendesha gari hilo akiwa amelewa.

“Uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo akiwa amelewa na kusababisha kupoteza umakini barabarani,” alisema Kamanda Maigwa.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa na Mkuu wa Shirika la Masista wa Veronica wa Uso Mtakatifu wa Yesu, Sista Jay Anni Cagoyong, amesema Sista Agatha atazikwa Agosti 2, 2025 kwenye Jumuiya ya Masista wa Veronica Malowa, Rombo.

“Adhimisho la misa takatifu ya mazishi litafanyika Jumamosi Agosti 2, 2025 kuanzia saa 5:00 asubuhi, kwenye Jumuiya ya Masista wa Veronica Malowa, Rombo, Jimbo Katoliki la Moshi,” imeeleza taarifa hiyo.

Mkuu wa Shirika la Masista Wafransiskani Wakapuchini wa Maua, Sista Christiana Njau, amesema katika taarifa yake kwamba Sista Calista atazikwa Agosti Mosi, 2025 katika makao makuu ya shirika Kilema, Wilaya ya Moshi.

“Adhimisho la misa takatifu ya mazishi itaadhimishwa Ijumaa Agosti Mosi, 2025 kuanzia saa 5:00 asubuhi, makao makuu ya shirika Kilema, Jimbo Katoliki Moshi,” imeeleza taarifa hiyo.

“Habari ziwafikie maaskofu, mapadre na watawa wa Jimbo Katoliki la Moshi, familia ya Sista Agatha Alphonce Shirima, ndugu, jamaa, marafiki na familia yote ya Mungu na wote wenye mapenzi mema. Raha ya milele umpe ee Bwana, na mwanga wa milele umwangazie, apumzike kwa amani,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo