Mapigano makali mpakani mwa Thailand na Cambodia

Dar es Salaam. Thailand na Cambodia zinashambuliana vikali katika mpaka unaotenganisha nchi hizo za bara la Asia, huku makumi ya watu wakiripotiwa kuuawa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya RFI, DW hadi sasa watu 33 wameshafariki dunia kutokana na mapigano hayo.

Mapigano hayo yamefikia siku ya tatu ambapo zaidi ya watu 168,000 wamekimbia makazi yao, huku shinikizo la kimataifa likiongezeka kwa pande zote mbili kufikia makubaliano ya kusitisha uhasama.

Mashambulizi ya makombora na risasi yameripotiwa karibu na vijiji kadhaa vilivyopo eneo la mpaka baina ya nchi hizo mbili, hali inayotanua eneo la mapigano tangu uhasama ulipozuka Alhamisi iliyopita.

Siku hiyo bomu la kutegwa ardhini lililipuka na kuwajeruhi wanajeshi watano wa Thailand. Kila upande umedai umechukua hatua ya kulipa kisasi kwa matendo yaliyofanywa na mwingine. Nchi zote mbili zimewaondoa mabalozi wake na Thailand imevifunga vituo vyote vya mpaka wake wa kaskazini mashariki na Cambodia.

Mamlaka nchini Cambodia zimetangaza vifo vya watu 14 wakati maofisa wa Thailand wamesema mwanajeshi wake mmoja ameuawa jana Jumamosi na kufanya idadi jumla upande huo kufikia vifo 20.

Hata hivyo, Jumuiya ya kikanda ya mataifa ya kusini mashariki mwa bara la Asia, ASEAN, inakabiliwa na shinikizo la kutafuta suluhu kati ya nchi hizo mbili wanachama.

Kwenye mkutano wa dharura ulioitishwa juzi Ijumaa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limeitolea wito kwa ASEAN kusuluhisha mgogoro kati ya Thailand na Cambodia.

Wizara ya Ulinzi ya Cambodia imekosoa kutanuka kwa mashambulizi ya Thailand mapema jana Jumamosi.

Imesema makombora makubwa matano yalirushwa na Thailand kuyalenga maeneo tofauti ya jimbo la Pursat, na kulitaja shambulizi hilo kuwa kitendo cha uchokozi na kilichopangwa makusudi.