Taylor arudi kivingine Mount Uluguru

DEREVA mkongwe, Frank Taylor ameamua kurudi katika mchezo wa mbio za magari na anatarajia kushiriki mbio za Mount Uluguru zitakazofanyika Agosti 16 na 17, mkoani Morogoro.

Taylor anakuwa miongoni mwa washiriki watano waliothibitisha kushiriki mbio hizo za raundi ya tatu na kufika 12 na anatarajiwa kutumia gari aina ya Nissan PA 10 ambayo wakati wa zama zake ilijulikana sana kama ‘Punda Afe Mzigo Ufike’ kutokana na uimara wake barabarani.

Madereva wengine waliothibitisha ushiriki wao hadi mwishoni mwa juma, ni Dharam Pandya na Tufail Amin kutoka Dar es Salaam, Diwani Hamid Mbatta kutoka Iringa na Gurpal Sandhu kutoka Arusha.

Dereva Charles Bicco na msoma ramani wake David Matete kutoka Amapiano ya Dar es Salaam, ndio waliokuwa washiriki wa  kwanza kujisajili kwa ajili ya mbio hizi, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Klabu ya Mount Uluguru, Gwakisa Mahigi.

Mahigi alisema anatarajia kupata zaidi ya washiriki 20 katika raundi hii wakiwemo Manvir Birdi, Randeep Singh na Shahzad Munge kutoka Dar es Salaam ambao wapo katika tano bora ya msimamo wa pointi katika kulitafuta taji la ubingwa wa taifa kwa mwaka huu.

Hadi mwisho wa raundi ya pili, Gurpal Sandhu alikuwa anaongoza mbio za ubingwa wa Taifa akifuatiwa na Manveer Birdi na Randeep katika nafasi ya pili waati Shehzad Munge akishikilia nafasi ya tatu akifuatwa na Dharam Pandya na Waleed Nahdi.

Katika mbio hizo, waandaaji wamesema watatoa ofa ya mafuta kwa kila mshiriki kwa ajili ya uhakiki wa njia pamoja na malazi.

Baada ya kuandaa raundi ya tatu ya ubingwa wa Taifa, Morogoro itakuwa tena mwenyeji wa raundi ya tano na ya mwisho ya mbio za ubingwa wa Afrika mwezi Septemba, mwaka huu.