Rombo. Mwalimu wa Shule ya Msingi Sinya, iliyopo Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Samwel Mlay (39), anadaiwa kujiua kwa kujiteketeza kwa moto katika nyumba yake aliyokuwa akiishi na familia yake.
Mwalimu Samwel Mlay (39) enzi za uhai wake
Mlay alikuwa akiishi katika Kijiji cha Ngoyoni kilichopo katika Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, chanzo cha kufikia uamuzi huo kikidaiwa kuwa ni mgogoro wa kimapenzi wa muda mrefu na mkewe.
Inadaiwa kuwa kabla ya kufanya tukio hilo, mwalimu huyo alimtoa nje mwanaye wa miaka minane na kisha kuwasha moto nyumba yake hiyo ambayo yote iliteketea yote.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema tukio hilo limetokea Julai 25, 2025 na kwamba mwanaume huyo alijifungia ndani na kisha kuwasha moto kwenye kochi lililokuwa sebuleni huku akiwa amejifunika blanketi.

“Huyu mwalimu alichukua uamuzi ya kujifungia ndani na baada ya hapo aliwasha moto kwenye kochi, akiwa amejiviringisha blanketi na kujitumbukiza kwenye moto huo,” amesema Kamanda Mkomagi.
Amefafanua kuwa juhudi za majirani na familia kumuokoa kwenye moto huo hazikuzaa matunda kwani waligundua wakati umeshatanda na kuwashinda nguvu. “Wakati wanatupa taarifa kuhusiana na tukio hilo tayari moto ulikuwa umeshatanda kwenye kubwa ndani ya nyumba hiyo.”
“Kwa mujibu wa taarifa zao, huyu mwalimu aliwasha moto saa 1 usiku na sisi tulikuja kupigiwa simu saa 2 usiku, hadi tunafika eneo la tukio, ulikuwa umekuwa mkubwa, tulitumia vifaa vyetu kuvunja na kuingia ndani na kuzima moto lakini tayari mwanaume huyo alikuwa amefariki,” amesema Kamanda Mkomagi.

Kamanda Mkomagi amesema: “Baada ya sisi kuchukua maelezo kwa Mtendaji wa Kijiji ni kwamba chanzo ni msongo wa mawazo uliomsababisha kuchukua uamuzi huo na huko nyuma aliwahi kusema kuwa atajiua.”
Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa majirani ambaye ni diwani mstaafu wa eneo hilo, Felician Kavishe amesema familia hiyo imekuwa na mgogoro wa muda mrefu.
“Mwalimu kwa muda mrefu alikuwa akimtuhumu mkewe kumsaliti. Walikuwa na ugomvi wa muda mrefu na walikuwa wakisumbuana sana na ilikuwa kiasi mwanaume alikuwa analewa kupita kiasi,” amedai jirani huyo.
Hata hivyo, amesema walipofika eneo la tukio walikuta moto ni mkubwa na hakuna hata kitu kimoja kilichosalia ndani ya nyumba hiyo.
“Wananchi walijaribu kuzima moto lakini hakuna kilichosalia, nyumba yote iliteketea kwa moto na jamaa aliungulia ndani na taarifa ni kwamba yeye ndiye aliyewasha moto ndani,” amesema jirani huyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ngoyoni, Frigilu Assenga amesema kabla ya tukio hilo mwalimu huyo alimtoa nje mwanaye wa miaka minane.
“Nilifika eneo la tukio na tulikuta tayari ameungulia ndani, bahati nzuri alichofanya alikuwa amemfukuza nje mtoto wa kike wa miaka minane na wakati huo mke wake alikuwa nje,” amesema mwenyekiti huyo.