Presha zaanza uchaguzi RT | Mwanaspoti

ZIKIWA zimebaki siku chache tu kabla ya kufanyika kwa usaili utakaofanyika Agosti Mosi, presha inazidi kupanda na kushuka kwa wagombea 20 waliochukua fomu ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

Usaili huo utafanyika jijini Dar es Salaam na utakuwa ni kipimo muhimu cha kuamua ni nani atapewa fursa ya kupambana katika uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 16, jijini Mwanza.

Wagombea hao 20 waliojitokeza watawania kiti cha Rais, Makamu wa Rais, Mwakilishi wa Wanawake na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji yenye nafasi nne, huku kila mmoja ana ndoto ya kushika hatamu za uongozi katika mojawapo ya vyama muhimu vya michezo hapa nchini.

Moja wa wagombea aliyezungumza na Mwanaspoti alisema japo presha inapanda na kushuka kwa sababu hajui ni maswali gani ataenda kuulizwa kwenye usahili lakini anaamini atatoboa kutokana na uzoefu wake katika mchezo wa riadha.

“Ni kweli huu ni mtihani wa maisha na hakuna hata mtu mmoja ambaye anataka kusikia jina lake limekatwa kwangu niko tayari na usaili,” alisema mgombea huyo jina limehifadhiwa.

Aliongeza usaili huo kwake ni hatua ya kuonyesha uwezo wake wa kiungozi na kujenga imani anaweza kuleta mageuzi katika riadha ya Tanzania.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa RT, Leonard Thadeo alisema wamewaelekeza wagombea wote waje na vielelezo ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kuthibitsha maelekezo ambayo walitoa kwenye fomu.

“Katika kupitia vielelezo hivyo tutapitia na kujiridhisha kama ni vielelezo halali au vya kugushi na wale ambao watakuwa wamewasilisha vya kugushi watakuwa wamepoteza sifa,” alisema Thadeo nyota wa zamani wa kimataifa aliyewahi kutamba na Yanga aliyeongeza;

“Wale ambao watakuwa na vielelezo halisi watakuwa na sifa za kuendelea na mchakato.”

Aliongeza mbali na wagombea kuwasilisha vielelezo, pia itategemea na hojaji zingine ambazo zitatumika siku hiyo ikiwemo maswali kulingana na maelekezo ya kikatiba na wale ambao watayajibu sawa sawa ukiunganisha na nyaraka walizonazo watawapitishwa kwa ajili ya kwenda kugombea.

Waliojitokeza kuomba uongozi katika uchaguzi huo na watakasailiwa hiyo Agosti Mosi ni Angelus Likwembe, Juma Ikangaa, Rogath John Stephen, William Kallaghe, Nsolo Mlozi na Silas Isangi wote wakiwani Urais, huku Baraka Sulus na Jackson Ndaweka wakijitoza nafasi ya Makamu wa Rais.

Wengine ni Noela Mafuru, Lwiza Msyani (Mwakilishi Wanawake), Christina Paga, Slyvia Rushokana, Shenya Imori, Alfredo Shahanga, Tullo Chambo, Michael Washa, Ibrahim Adam, Andrew Rhobi, Tabu Mwandu na Joshua Kayombo wanaowajia nafasi nne za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.