Askofu Gwajima ashikwa kigugumizi kisa ubunge, kushiriki vikao CCM

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amevunja ukimya kuhusu sababu ya yeye kutojitosa na kutangaza nia ili kutetea ubunge wa Kawe katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi leo Jumapili, Julai 27, 2025, kiongozi huyo ameeleza kinachozungumzwa hivi sasa kumhusu yeye kutoonekana kwenye mikutano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), akiwa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC).

Licha ya kuwawakilisha wananchi wa Kawe kwa miaka mitano, Askofu Gwajima si miongoni mwa makada wa CCM waliochukua fomu ya kuomba tena ridhaa ya kuwania ubunge, huku hata kwenye vikao ambavyo yeye ni mjumbe hakuonekana.

Askofu Gwajima amesema hayo jijini Dar es Salaam leo, Jumapili, Julai 27, 2025, katika mahojiano na Mwananchi, ikiwa ni siku moja kupita tangu kufanyika vikao viwili vikubwa vya Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mkutano mkuu, ambavyo naye ni mjumbe.

Katika kikao cha NEC na mkutano mkuu maalumu, ambavyo vyote vilifanyika kwa mtandao jana Jumamosi, Julai 26, 2025, Askofu Gwajima hakushiriki.

Alipoulizwa kwanini hakuchukua fomu kutetea kiti chake cha ubunge wa Kawe, alivuta pumzi ndefu na kurudia kuitaja Kawe mara tatu, kisha akajibu kwa ufupi kuwa ni raha kwake kuwa askofu na kuhubiri Injili.

“Kurudi Kaweee, mimi kurudiii Kaweee, aaaaaah, ninaomba nikae kimya kwenye hilo, no answer (hakuna jibu), ila ninachoweza kusema ni raha sana kwangu kuwa askofu na kuhubiri Injili,” amesema.

Katika mchakato wa ndani wa uchukuaji na urejeshaji fomu ndani ya CCM, Askofu Gwajima hakujitosa kutetea nafasi hiyo.

Katika mahojiano hayo, Gwajima amejibu kuhusu kutohudhuria kwake vikao na mikutano ya chama chake, akisema yupo nchini na atakapopata nafasi atakwenda kwenye shughuli za chama chake.

“Nipo, na kwenye mikutano nikipata nafasi nakwenda bila wasiwasi. Mimi ni mwanachama wa CCM,” amesema.

Askofu Gwajima siku za karibuni alionekana kwenye picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), aliyeshambuliwa na kitu kizito Mei mosi, 2025.

Katika picha hiyo, aliyoichapisha katika ukurasa wake wa Instagram, Askofu Gwajima aliandika: “Leo Juni 2025 nimepata nafasi ya kumtembelea na kumjulia hali Padre Dr. Charles Kitima, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).”

Kutokana na picha hiyo, Askofu Gwajima ameulizwa walizungumza nini walipokutana, amejibu: “Naomba nisilizungumzie, libaki kama lilivyo.”

Kanisa la Ufufuo na Uzima, analolihudumu kama Askofu Mkuu, lilifutwa na kuzungushiwa utepe tangu Juni 3, 2025, kwa kile kilichoelezwa katika moja ya barua kuwa limevunja taratibu kwa kuhusisha mambo ya siasa.

Baada ya kufutwa, Jeshi la Polisi lilikwenda kanisani hapo, kuzungusha utepe na kulinda ili waumini wasiendelee na ibada kanisani hapo.

Uamuzi wa kufutwa kwa kanisa hilo ulitangazwa na Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa, kwa kile alichoeleza kuwa ni kukiuka Sheria ya Jumuiya Sura ya 337, “kwa kutoa mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha Serikali na wananchi.”

Hata hivyo, waumini na viongozi wa kanisa hilo wamefungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo wa kufutwa kwa kanisa hilo lenye makanisa zaidi ya 2,000 nchini.

Aidha, waumini hao wamekuwa wakihama-hama ili kufanya ibada ya Jumapili, huku wakitawanywa mara kadhaa na kupigwa mabomu ya machozi, kabla ya hivi karibuni kufanya ibada hiyo kwenye moja ya kumbi eneo la Kimara.

Ibada hiyo ilihudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando, ambaye katika hotuba yake alisema anatamani suala la waumini hao liishe.

Kuhusu yote yaliyoendelea kanisani kwake, Askofu Gwajima amesema ana mengi ya kuzungumza lakini kwa kuwa yeye ni kiongozi, atafanya hivyo kwa tahadhari.

Hata hivyo, amesema atazungumza pale itakapolazimu kufanya hivyo, na kwamba ataongeza sana itakapobidi.

Lakini kwa hatua ya sasa, amesema naye anatamani suala hilo liishe kwa watu kuruhusiwa kuabudu, na kwamba amemsikia Msando.

“Nilimsikia mkuu wa wilaya, lakini nikasema kesi ipo mahakamani. Mkuu wa wilaya ataingiliaje? Namhurumia Msando kwa sababu lipo kwenye eneo lake, lakini anaweza kulimalizaje suala ambalo lipo mahakamani?

“Angesema labda amepewa maelekezo na mamlaka kwamba tufungue kanisa chini ya masharti haya na haya, sawa. Lakini kwa vile alivyosema na suala lipo mahakamani, alichokisema kwa waumini, naona ni kupoteza muda tu,” ameeleza.

Amesema Msando ana namba yake ya simu, angempigia akamshauri kwa kumuelekeza katika kumaliza changamoto ya waumini.

“Cha kujiuliza kingine ni kwamba, hili halikusababishwa na mkuu wa wilaya. Anaweza kulimalizaje? Mwenye uwezo huo ni Waziri wa Mambo ya Ndani (Innocent Bashungwa), kuandika barua ya kufungua kanisa,” amesema.

Askofu Gwajima amesema maaskofu wake walikutana na mkuu wa wilaya, kisha wakampa mrejesho wa kile walichozungumza.

“Waliniambia katika mazungumzo yao alisema hajaagizwa na mtu, ni mawazo yake. Kama angekuwa ameagizwa kutaka ili suala liishe, sawa. Kwani hata sisi tunapenda liishe, na kuisha kwake ni kufungua kanisa. Nafahamu taratibu, aliyelifunga kanisa ni msajili. Mkuu wa wilaya analimalizaje?” amehoji.

Hata hivyo, amesema anashindwa kuongeza kuhusu waumini wake kusumbuliwa wanapoabudu, akisema yeye ni kiongozi, hivyo akizungumzia hilo kutaleta shida.

“Hata nilipofanya press (mkutano na waandishi) ya kwanza sikuongea kabisa kuhusu kanisa na ule uonevu uliofanyika. Mimi ni kiongozi, nikiongea italeta shida.

“Mfano, ni mtu tu alisema hao watu (waumini) wanakwenda kuabudu Kanisa la Kilutheri, kanisa lote likavunjwa eti lipo karibu na barabara. Lakini pembeni yake kuna huduma nyingine zinaendelea,” amedai.