MABOSI wa Singida Black Stars wamempa ‘Thank You’, Jonathan Sowah kubariki kutua Simba, huku hesabu zikiwa ni kumbeba mshambuliaji wa Berekum Chelsea ya Ghana kwa ajili ya msimu ujao, lakini ghafla dini hilo limetibuka baada ya nyota huyo kubadilisha mawazo ya kuja Tanzania baada ya kumalizana na Smouha ya Misri.
Amankonah alihitajika Singida kwa ajili ya kuchukua nafasi ya mshambuliaji mwenzake raia wa Ghana, Jonathan Sowah ambaye inaelezwa anaweza kujiunga na Simba, jambo ambalo kwa sasa limewavuruga mabosi wa kikosi hicho kusaka tena mbadala wake.
Sowah aliyejiunga na Singida dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya, alifunga mabao 13, ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, jambo lililozivutia klabu mbalimbali kwa ajili ya kuipata saini ya mshambuliaji huyo.
Pia, Sowah ameiwezesha timu hiyo kumaliza katika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 57 na kufuzu michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu ujao, huku akiifikisha fainali ya Kombe la FA na kuchapwa mabao 2-0 na Yanga.
Mmoja wa viongozi wa Singida, aliliambia Mwanaspoti chaguo la kwanza lilikuwa kwa Amankonah kutokana na uwezo alionao, japo kwa sasa imekuwa tena vigumu baada ya kutua Misri, hivyo wanasubiri mapendekezo mapya ya benchi lao la ufundi.
“Kocha wetu, Miguel Gamondi atawasili Tanzania muda wowote hivyo, tunasubiri atupe tena mapendekezo yake katika eneo la ushambuliaji, Elvis Rupia yupo ila kama ataondoka Sowah maana yake ni lazima tuzibe nafasi yake,” kilisema chanzo hicho.
Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Ismaily ya Misri, zilimuhitaji pia mshambuliaji huyo ambaye msimu wa 2024-2025 wa Ligi Kuu ya Ghana, aliibuka mfungaji bora, baada ya kufunga mabao 15.
Tuzo hiyo ya ufungaji bora kwa Amankonah, ni ya pili mfululizo baada ya msimu wa 2023-2024, kuichukua kufuatia kufunga mabao 19, akimzidi, Steven Dese Mukwala anayeichezea Simba kwa sasa aliyefunga mabao 14, wakati akiwa na Asante Kotoko.
Amankonah mwenye miaka 25, ametetea tuzo yake ya ufungaji bora kwa misimu miwili mfululizo, huku akiiwezesha pia Berekum Chelsea kumaliza nafasi ya 12, katika Ligi Kuu ya Ghana na pointi 44, ikishinda mechi 12, sare minane na kupoteza 14.