Dar es Salaam. Baada ya kubainika uwepo wa watu kujiandikisha zaidi ya mara moja kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura, imeelezwa kuwa, kutojua sheria sio kinga mbele ya sheria. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Jacobs Mwambele watu 8,703 wamebainika kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Imeelezwa kuwa, kufanya hivyo ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 Kifungu cha 114 (b) kinachozuia mpigakura kujiandikisha zaidi ya mara moja.
Pia, muhusika akithibitika atakabiliwa na adhabu ya kulipa faini isiyopungua Sh100,000 na isiyozidi Sh300,000 au kifunguo kati ya miezi sita na miezi 24 au vyote kwa pamoja.
Kufuatia hilo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima jana Jumamosi alikabidhi kwa polisi nakala ngumu na tete ya majina hayo na kueleza kuwa, wamevunja sheria kwa mujibu wa miongozo.
Alisema Watanzania hao wamechukuliwa picha, alama za vidole, vituo walivyojiandikisha na namba za simu, jambo linalokwenda kuwarahisishia polisi katika kuwatambua.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Julai 27, 2025, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime amesema watatumia mbinu zote za kitaalamu ikiwamo kushirikiana na wadau mbalimbali na wananchi ili kuhakikisha mkono wa sheria unawafikia haraka iwezekanavyo.
“Mtu yeyote anayejiandikisha zaidi ya mara moja kwenye Daftari la Wapigakura, sheria ipo wazi kwamba, anafanya kosa la jinai na hatua stahiki ni kukamatwa na kulingana na ushahidi atafikishwa mahakamani,” amesema Misime.
Hata hivyo, Jaji Mwambele ameiambia Mwananchi kuwa watu hao hawatatolewa kwenye orodha ya wapigakura ila majina yao yatabaki pale walipojiandikisha mara ya mwisho, ndipo watakaporuhusiwa kupigia kura.
Kifungu cha 114 (b) cha sheria hiyo ni kosa kwa mtu kwa kujua au akiwa na sababu ya kuamini kuwa, ameandikishwa katika eneo la uchaguzi halafu akaenda kujiandikisha eneo lingine.
Kifungu hicho kinaeleza kuwa, endapo mtu atafanya hivyo tena bila kueleza kwa ofisa mwandikishaji kuhusu uandikishwaji wake wa awali, atakuwa amefanya kosa na akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua Sh100,000 na isiyozidi Sh300,000 au kifunguo kati ya miezi sita na miezi 24 au vyote kwa pamoja.
Adhabu ya aina hiyo inaweza kumkumba pia mtu ambaye ameomba kuandikishwa katika eneo la uchaguzi wakati tayari alishaomba kuandikishwa eneo lingine la uchaguzi na maombi yake ya awali hayajaamuliwa kwa kusubiri uchunguzi wowote kuhusu sifa ya mwombaji au kuondolewa.
Kwa mujibu wa wanasheria, iwapo uchunguzi wa polisi utathibitisha uandikishaji mara mbili ulifanywa kwa makusudi, wahusika wanaweza kufikishwa mahakamani na kukabiliwa na adhabu kali kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na Mwananchi, Wakili Aloyce Komba amesema kifungu hicho kinaweza kuwafanya watu wengi wakwepe kujiandikisha kwenye chaguzi zijazo kwa kuhofia kukutana na adhabu kali.
Amesema kwa Tanzania, suala la kujiandikisha kwenye orodha ya kupiga kura na kitendo chenyewe cha kupiga kura, sio kosa kisheria, hivyo wapo watakaoona ni heri wajiweke mbali na mchakato huo kuliko kwenda kukumbana na adhabu ya kujiandikisha zaidi ya mara moja.
“Kutojua sheria sio utetezi, lakini tujiulize je! Wananchi walielimishwa vya kutosha? Inawezekana kabisa wapo waliojiandikisha kwa nia njema, labda alitoka eneo moja kwenda jingine lakini kwa kukosa elimu akajikuta anajiandikisha mara ya pili.
“Kuna lawama nazipeleka kwa Tume kwa sababu wana wajibu wa kutoa elimu kwa umma, lakini pia watanzania nao wajifunze kutafuta taarifa, inawezekana usipate elimu kutoka INEC, lakini kupitia kusoma, kuuliza, unaweza kujua kwamba kujiandikisha zaidi ya mara moja ni kosa kisheria,” amesema Komba.
Hoja hiyo imeungwa mkono na Mwanasheria Mary Mlata ambaye amesema wengi wanaoingia kwenye makosa kama hayao hufanya hivyo kwa kukosa uelewa wa sheria, lakini hiyo haiwezi kuwa utetezi.
“Kisheria, mtu anapaswa kuwa mwangalifu. Mara tu unapopata taarifa kuwa umeandikishwa, unapaswa kuepuka kujiandikisha tena, hata kama ni kwa nia ya kuhama kituo. Kuna taratibu maalumu zinazopaswa kufuatwa,” amesema Mary.
Hata hivyo, mwanasheria huyo amesema vitendo hivyo vinaashiria changamoto ya elimu kwa wapigakura nchini na akapendekeza INEC kuongeza juhudi za kutoa elimu ya mpiga kura.
“Ni wazi kuwa, baadhi ya watu hawa walifanya kwa makusudi, lakini huenda wengine walifanya kwa kutoelewa. Hata hivyo, sheria haiangalii nia, bali matendo,” amesema.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Erick Ishengoma amesema suala la uandikishaji mara mbili linahatarisha uhalali wa mchakato wa uchaguzi na ni tishio kwa misingi ya demokrasia.
“Kujiandikisha mara mbili ni sawa na kujaribu kupiga kura mara mbili, jambo linalovuruga misingi ya uchaguzi huru na wa haki. Hili si kosa dogo, linapaswa kushughulikiwa kwa ukali ili iwe fundisho kwa wengine,”amesema Ishengoma.