Mbeya. Vilio na simanzi vimetawala katika Shule ya Sekondari Chalangwa, wilayani Chunya mkoani Mbeya, wakati wa kuagwa kwa miili ya wanafunzi sita waliopoteza maisha katika ajali ya basi, walipokuwa wakifanya mazoezi ya utimamu wa mwili.
Ajali hiyo ilitokea jana Jumamosi Julai 26, 2025 katika eneo la Chalangwa baada ya basi la abiria la Kampuni ya Safina Coach lililokuwa likitokea Chunya kuelekea Mbeya, kuwagonga wanafunzi hao na kusababisha vifo sita na kujeruhi wengine tisa.
Leo shule hiyo imegeuka uwanja wa majonzi wakati wa ibada ya kuwaaga marehemu hao huku viongozi wa Serikali na wananchi wakitoa pole na ushauri kuhusu usalama barabarani.
Wanafunzi waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni Seleman Msekwa, Kenedy Masoud , Samwel Zambi, Kelvin Mwasamba, Hosea Mbwilo na Amina Ulaya. Waliopata majeraha ni Benard Mashaka, Lilian Raymond, Vicent Baraka Malema, Siwema Nasibi Simbilo, Alex Peter, Dethani Charles, Getruda Mwakyoma na Farida Mwasongole.
Serikali imetangaza kugharamia mazishi ya wanafunzi hao na kugharimia matibabu ya majeruhi wote.
Aidha, imetoa agizo la kusitishwa kwa mazoezi ya ‘jogging’ barabarani kwa wanafunzi na vikundi vya michezo, ikiwa ni tahadhari ya kuzuia ajali kama hiyo.
Kati ya walioguswa na msiba huo ni baba mlezi wa mmoja wa marehemu, Kedron Mbwilo aliyempoteza mtoto wake wa kidato cha tatu. “Ni pigo kubwa kwa familia yetu kumpoteza mtoto ambaye tulimtegemea kwa maisha ya baadaye. Tunaishukuru Serikali kwa kuungana nasi katika wakati huu mgumu,” amesema kwa huzuni mzazi huyo.
Akizungumza msibani hapo, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbaraka Batenga ametoa wito kwa waendeshaji wa vyombo vya moto kuheshimu sheria za usalama barabarani na kuwa makini katika matumizi ya barabara.
“Uzembe wa madereva umekuwa chanzo kikuu cha ajali. Madereva wafahamu kuwa vyombo wanavyoendesha vinabeba uhai wa watu, wanapaswa kuwa makini sana,” amesema Batenga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Adam Mwakamalisya ameeleza masikitiko yake kuhusu ajali hiyo huku akisema tayari walishapokea malalamiko dhidi ya basi hilo.
“Basi hili tayari lilishaligonga gari la halmashauri siku za nyuma. Sasa limetokea tukio hili la kusikitisha. Tushirikiane kumtafuta dereva huyo ili achukuliwe hatua za kisheria,” amesema Mwakamalisya.
Wananchi pia wamezungumzia ajali hiyo na kuitaka Serikali na Jeshi la Polisi upande wa usalama barabarani, kuchukua hatua kali zaidi kwa madereva wanaosababisha ajali barabarani.
Akizungumzia hilo mkazi wa Chunya, Geoffrey Mwankenja amewataka madereva kuwa makini kabla ya kuyapita magari mengine hasa maeneo ya makazi ya watu.
“Ajali nyingi hutokea kwa uzembe wa madereva, Serikali ifuatilie kwa ukaribu,” amesisitiza mwananchi huyo.
Naye Ndomba Ndomba, mkazi wa Matundasi ameliomba Jeshi la Polisi kuendelea kufanya ukaguzi wa mabasi mara kwa mara.
“Eneo la ajali lilikuwa na alama za onyo, dereva alipaswa kuwa makini. Ukaguzi wa mabasi usisubiri ajali; ufanyike kwa kushtukiza ili kubaini madereva wasio na sifa,” amesisitiza.
Tukio hili limeacha majonzi si tu kwa familia za wanafunzi hao, bali kwa jamii nzima ya Chalangwa na Taifa kwa ujumla, huku wito ukiendelea kutolewa kwa wadau wote kuimarisha usalama wa barabarani na kulinda maisha ya Watanzania.