Rais Samia kufungua kongamano la elimu bila kikomo

Dodoma. Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) itawakutanisha wadau wa elimu katika maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, huku miongoni mwa malengo yakielezwa ni kuangazia umuhimu wa kujua kusoma na kuandika katika kujifunza bila ukomo.

Mbali na hilo, Rais Samia Suluhu Hassan atafungua kongamano la masuala ya elimu bila kikomo litakalofanyika Agosti 25, 2025 jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya TEWW.

Ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha ongezeko la idadi ya watu wanaojua kusoma na kuandika kutoka asilimia 72 ya mwaka 2012 hadi asilimia 83, mwaka 2022.

Akizungumza kuhusu maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo leo Julai 27, 2025, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu ya “elimu bila ukomo kwa maendeleo endelevu”.

“Sambamba na hayo, maadhimisho haya yanalenga kuangazia umuhimu mkubwa wa kujua kusoma na kuandika katika kujiendeleza kujifunza bila kikomo,” amesema.

Amesema lengo ni kuamsha ari miongoni mwa vijana na watu wazima ya kupata masuala ya ujasiriamali na ufundi wa awali.

Profesa Mkenda amesema dhana ya elimu ya watu wazima ni elimu bila ukomo na si suala la kujua kusoma na kuandika tu ni pamoja na kutoa na kupata ujuzi unaohitajika.

“Hiyo ni pamoja na elimu ya fedha, ujasiriamali na shughuli nyingine za kilimo. Kwa sababu kampeni ya elimu ya watu wazima wakati huo ikiitwa ngumbaru mtu anafikiria ni kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu lakini Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima inafanya zaidi ya hapo,” amesema.

Amesema hiyo ndiyo maana inatoa elimu nje ya mfumo rasmi huku akitolea mfano wa walioacha shule kwa sababu mbalimbali ambao wamekuwa wakipata elimu kupitia taasisi hiyo.

“Kilele cha maadhimisho hayo yatakayotanguliwa na shughuli mbalimbali kitakuwa Agosti 25 hadi 27, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam,”amesema.

Profesa Mkenda amesema zaidi ya wananchi na wadau 1,000 wa elimu kutoka ndani na nje ya nchi watakutana katika kongamano la masuala ya elimu bila ukomo.

Amesema mgeni rasmi atakayefungua kongamano hilo Agosti 25, 2025 atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan na litafungwa Agosti 27, 2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Dk Doto Biteko.

Profesa Mkenda amesema maadhimisho hayo yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo maofisa magereza wanaoendesha programu za kisomo magerezani na wakufunzi wakazi wa TEWW.

Amesema hayo yatafanyika Julai 28 hadi 30, 2025 jijini Dodoma na yatahusisha maofisa magereza na wakufunzi wakazi wa TEWW.

Amesema, pia, kutakuwa na maonyesho na huduma mbalimbali za elimu ya watu wazima yatakazofanyika kuanzia Agosti 24 hadi 27, 2025 katika ukumbi wa JNICC.

Mmoja wa wadau wa elimu, Jesca Mwadabila amesema uwepo wa taasisi hiyo umekuwa msaada kwa watu wazima wanaotaka kujiendeleza kmasomo.

“Kuna umri ambao huwezi kukaa tena darasani kwa muda mrefu ama hukupata alama zinazokuwezesha kuendelea na masomo ni rahisi kwenda Taasisi (TEWW) na kujiandikisha kwa ajili ya kuyarudia na wanakusaidia katika kufikia lengo lako,” amesema.