KAMA mabosi wa Yanga wangechelewa kidogo tu, ilikuwa inakula kwao baada ya beki wa kulia wa timu hiyo, Israel Mwenda kubakiza hatua chache kuchukuliwa, lakini mabingwa hao wakapindua meza.
Mwenda aliyekiowasha vizuri ndani ya miezi sita tu ya mkopo akitokea Singida Black Stars, alikuwa na hesabu za kuondoka Yanga baada ya kuona jambo lake la kusaini halimaliziki.
Wakati Yanga inapambana kimaslahi na beki huyo, kumbe Singida bado ilikuwa inamtamani, lakini Simba ambao ilikuwa inataka kumpa mkataba wa mwaka mmoja beki Shomari Kapombe, ili Mwenda akapewe mkataba wa muda mrefu zaidi.
Hata hivyo, Yanga ilishtukia hesabu hizo za Singida na Simba ambapo juzi ikamuita mezani tena na kupambana naye akikubali kusaini mkataba mpya.
Mwenda atasaini mkataba wa miaka mitatu akienda sasa kuwa mchezaji halali wa Yanga ukiondoa ile miezi sita ya kwanza aliyoitumikia kwa mkopo.
“Tumekubaliana atasaini mkataba wa miaka mitatu kubaki Yanga, mazungumzo yalikuwa magumu kabla lakini tumefanikiwa kuelewana na muafaka umepatikana,” alisema bosi huyo wa juu ndani ya Yanga.
Yanga itakapombakisha Mwenda inakwenda kupata uhakika wa beki wa maana upande wa kulia akisaidiana na Kibwana Shomari, wakati Yao Kouassi akiendelea kupona taratibu majeraha aliyonayo yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu sasa Jangwani.
Mwenda anakuja mchezaji wa nne wa kikosi kilichopita kutangazwa kuongezwa mkataba baada ya Mudathir Yahya, Pacome Zouzoua na Denis Nkane, huku nyota wapya waliotambulishwa ni Celestin Ecua, Lassane Kouma, Balla Mousa Conte na Mohamed Doumbia.