DILI la Simba la kutaka kumnasa winga wa kushoto wa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Thapelo Maseko linaonekana kuingia katika ushindani mpya baada ya klabu ya Aris Limassol ya Cyprus kuonyesha nia ya kumsajili nyota huyo kijana.
Kwa mujibu wa taarifa inaelezwa Aris tayari wameanza mazungumzo ya awali kuhusu ada ya usajili na masharti binafsi ya kumchukua Maseko, ambaye pia anawaniwa na vigogo wa Afrika Kusini Kaizer Chiefs na SuperSport United.
“Wameulizia kuhusu gharama ya kumsaini pamoja na masuala ya kimkataba. Kwa sasa, inaonekana dili la Cyprus lina uzito zaidi ukilinganisha na vilabu vya ndani,” kilisema chanzo hicho.
Taarifa hizi zinaweka presha kwa Simba, ambayo imedaiwa kuingia mazungumzo ya moja kwa moja na nyota huyo kupitia ushawishi wa kocha Fadlu Davids, ambaye anatokea pia Sauzi.
Simba ilikuwa na matumaini ya kumleta Maseko kama sehemu ya kikosi kipya kitakachosaidia klabu hiyo kurejesha heshima yake katika michuano ya ndani na kufanya vizuri kimataifa.
Lakini kwa sasa, ushindani kwenye dili hili unazidi kuongezeka. Aris Limassol, klabu anayochezea pia mchezaji mwingine kutoka Afrika Kusini, Mihlali Mayambela inaonekana kuwa na faida zaidi ya kuvutia kinda huyo ikiwemo kupata fursa ya kucheza Ulaya.
Maseko, aliyezaliwa Sebokeng, amekuwa akipambana kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza cha Sundowns chini ya kocha Miguel Cardoso na msimu uliopita alicheza mechi 14 tu katika mashindano yote kwa dakika 346.
Hata hivyo, aliibuka kuwa Mchezaji Bora wa Mashindano ya African Footbal League (AFL), na pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Bafana Bafana kilichoshinda medali ya shaba AFCON 2023 huko Ivory Coast.