Fadlu abeba mbadala wa Tshabalala

LICHA ya kuongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia Namungo, beki wa kushoto Anthony Mligo yupo katika rada za Kocha wa Simba, Fadlu Davids anayedaiwa kuwaambia mabosi wa timu hiyo kuwa anahitaji huduma ya kijana huyo mwenye miaka 20, kiasi cha kumuita mazoezini amuone zaidi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Simba, siku ya Alhamisi iliyopita, mchezaji huyo alikutana na viongozi wa juu wa klabu hiyo na kualikwa kushiriki nao mazoezi kama sehemu ya kumtathmini kwa ukaribu.

Hata hivyo, licha ya uwepo wake uwanjani kwa mazoezi, hakuna hatua ya makubaliano iliyofikiwa baina ya pande hizo mbili kuhusu usajili wake.

Taarifa kutoka kwa watu wa karibu na mchezaji huyo, zinasema baada ya kuona hakuna mawasiliano ya maana yanayoendelea kutoka upande wa Simba, Mligo aliamua kurejea Namungo, timu ambayo imeonyesha kuwa tayari kumuachia endapo Simba itaonyesha nia ya kweli kwa kutuma ofa rasmi.

Kocha Fadlu, aliye katika maandalizi ya mwisho ya safari ya kikosi hicho kwenda Ismailia, Misri kwa maandalizi ya msimu, alionekana kushangazwa na kutokuwepo kwa Mligo mazoezini juzi Jumamosi, jambo lililodhihirisha kuwa bado anamhitaji mchezaji huyo licha ya kimya kutoka kwa viongozi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Fadlu ametoa msimamo wa wazi kwa uongozi wa Simba kwamba Mligo ni chaguo lake katika nafasi ya beki wa kushoto na amewataka kuhakikisha kuwa mchezaji huyo anakuwa sehemu ya kikosi kitakachosafiri kwa ‘pre-season’.

Simba tayari inatajwa imekamilisha usajili wa mabeki wawili wa kushoto mmoja akiwa ni mzawa, Miraji Abdallah ‘Zambo’ kutoka Coastal Union na mwingine kutoka klabu ya Al Hilal ya Sudan, lakini hilo halijamfanya Fadlu abadili msimamo kuhusu Mligo. Fadlu anamuona Mligo kama mbadala sahihi wa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.

Kwanini? inaelezwa kuwa anaamini ana uwezo wa kuchangia kitu tofauti katika kikosi chake, hasa kutokana na ujana wake, kasi, nidhamu na uwezo wa kushambulia kutoka pembeni.

Mligo ni miongoni mwa mabeki waliovutia msimu uliopita akiwa na Namungo. Anasifika kwa utulivu akiwa na mpira miguuni, kushambulia na kurudi kwa kasi katika eneo lake la ulinzi.

Simba imeondokewa na mabeki wawili waliokuwa wakitumika mara kwa mara katika upande wa kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye alikuwa nahodha wa kikosi hicho  na Valentin Nouma hali iliyoacha pengo katika eneo hilo.

Kocha Fadlu ameanza kulijenga upya eneo hilo kwa kusajili wachezaji wapya, lakini bado anaamini kuwa uwepo wa Mligo unaweza kuongeza ushindani na kutoa chaguo bora zaidi katika kikosi chake.