Mpinzani wa Rais Biya azuiwa kushiriki uchaguzi mkuu

Dar es Salaam. Wakati ikiwa imesalia miezi miwili kabla ya kufanyika kwa uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, Maurice Kamto mpinzani wa Rais wa Cameroon Paul Biya amezuiwa kushiriki uchaguzi huo.

Rais Biya mwenye umri wa miaka 92, yeye atagombea tena mwaka huu ikiwa ni muhula wa nane wa uongozi katika nchi hiyo. Biya ndiye Rais mwenye umri mkubwa zaidi duniani na anaweza kusalia madarakani hadi atakapofikisha miaka 100 iwapo atashinda uchaguzi huo.

Jina la Kamto, mpinzani mkuu wa Rais Biya, halijarudishwa na Tume ya Uchaguzi ya Cameroon kugombea jambo ambalo limezua hofu ya ghasia na kuongeza uwezekano wa ushindi mwingine kwa rais huyo aliyeko madarakani kwa miongo kadhaa.

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi, ELECAM, alitangaza uamuzi huo katika mkutano na waandishi wa habari Jumamosi aliposoma orodha ya wagombea 13 walioidhinishwa, ambayo haikumjumuisha Kamto.

Hakuna sababu zilizotolewa kwa ajili ya kutengwa kwake, na wale ambao hawakuorodheshwa wana siku mbili za kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo. Kwa mujibu wa Al Jazeera na DW.

Kamto, mwenye urmi wa miaka 71, alikuwa amewasilisha rasmi ugombea wake wiki iliyopita, alionekana kuwa mpinzani mkali zaidi wa Biya katika chaguzi zilizopita.

Ni majina 13 tu kati ya 83 yaliyowasilishwa kwa tume ya uchaguzi cha nchi hiyo, Elecam ambayo yalikubaliwa.

Alishika nafasi ya pili wakati wa uchaguzi uliopita wa 2018 kwa asilimia 14 ya kura, wakati Biya, ambaye anaonekana kwenye orodha ya uchaguzi, alishinda kwa urahisi na zaidi ya asilimia 70 katika uchaguzi uliokumbwa na madai ya udanganyifu na idadi ndogo ya wapiga kura.

Kamto alitaka kugombea kwa chama cha kikomunisti cha African Movement for New Independence and Democracy (MANIDEM). Katika uchaguzi wa 2018, Kamto alisimama kwa chama chake mwenyewe, Cameroon Renaissance Movement (MRC), ambacho alikianzisha mwaka 2012.

Miongoni mwa wagombea wengine walioidhinishwa kugombea katika uchaguzi ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Bello Bouba Maigari, mshirika wa Biya kwa karibu miaka 30, na Issa Tchiroma Bakary, ambaye alijiuzulu kama waziri wa ajira mapema Juni ili kuwasilisha ugombea wake.