Kachwele: Kucheza na Messi kumeniongezea kitu

MSHAMBULIAJI wa Whitecaps anayecheza kwa mkopo Vancouver Whitecaps inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani (MLS), Cyprian Kachwele amesema kucheza ligi moja na Lionel Messi (Inter Miami) kumemwongezea uzoefu.

Kinda huyo wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ aliyewahi kupita timu ya vijana ya Azam FC, huu ni msimu wake wa pili Marekani na msimu uliopita akiwa na kikosi cha timu ya wachezaji wa akiba ya Whitecaps FC 2 alicheza mechi 21 na kufunga mabao matano.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kachwele alisema ingawa hajacheza na Messi, kuwepo kwenye ligi hiyo kwake anajifunza vitu vingi hasa kupambana.

“Sijabahatika kucheza naye kwa sababu nilikuwa na majeraha, lakini namwona sababu ni ligi moja. Ni mchezaji ambaye najifunza vitu vingi kutoka kwake kwani amefanya makubwa duniani,” alisema Kachwele.

Aliongeza, amepona na tayari amerudi uwanjani na wiki iliyopita alicheza mechi ya kwanza baada ya kutoka majeruhi akifunga bao moja na kutoa asisti.

“Nilikuwa na changamoto ya jeraha la paja, lakini nashukuru Mungu nimerejea haraka na wiki iliyopita nilicheza mchezo wangu wa kwanza, nikafunga.”