Rukwa. Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limewakamata wanachama 11 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiwamo viongozi wanne kwa madai ya kufanya mkusanyiko usio halali.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 28, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Shadrack Masija amewataja waliokamatwa kuwa ni Winifrida Joseph Khenani (Katibu Mwenezi wa Bavicha Jimbo la Nkasi Kaskazini), Godfrid Bendera (Katibu wa Chadema wa jimbo hilo), Evarist Mwanisawa (Katibu wa Baraza la Wazee Chadema Wilaya ya Nkasi), na Scolastica Mwalonde (Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Majengo).
Pia, Jeshi la Polisi limewataka mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani na Albeto Kaliko maarufu Galincha (aliyekuwa diwani wa kata ya Itete), kujisalimisha Polisi Wilaya ya Nkasi au ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Rukwa kwa kupanga mkusanyiko huo usio halali.
Kamanda Masija amesema kufuatia kukamatwa wanachama hao, wameibuka watu wanaotuma taarifa za uongo, upotoshaji na za kubuni kwenye mitandao ya kijamii wakiwa na lengo la kuitia hofu jamii au kulichonganisha jeshi hilo na wananchi.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa linamtaka Alfred Sotoka kuripoti Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Rukwa kufuatia kutuma taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na tukio hilo.
“Ninamtaka Sotoka kujisalimisha wala usijifiche, kwani utasakwa popote ulipo,” amesema Kamanda Masija. Pia, amewataka wananchi kufuata sheria wanapotaka kufanya mkusanyiko.
Kamanda huyo amesema wananchi wanatakiwa kutumia vizuri mitandao ya kijamii na ya mawasiliano kwa kuacha tabia za kutoa au kusambaza taarifa wasizo na uhakika nazo.
Akizungumzia sakata la Khenani na wenzake akiwa Mahakama ya Kisutu, jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amedai mbunge huyo alivamiwa na polisi na kupigwa.
“Mbunge wetu amevamiwa nyumbani kwake na Jeshi la Polisi kwa madai kwamba kuna zuio la chama kufanya shughuli za siasa. Polisi wamempiga pamoja na watu wengine.
“Wameingia ndani ya nyumba yake, wamechukua baadhi ya mali zake, wameharibu kamera zake kwa madai kwamba kesi ya Chadema inazuia shughuli za kisiasa za chama,” amesema.
Heche amesema tayari chama hicho kimetuma jopo la mawakili mkoani Rukwa kushughulikia tatizo hilo, akisisitiza Chadema itamfungulia kesi Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nkasi ili akaeleze mahakamani alichokifanya.
Amesema haiwezekani Jeshi la Polisi kuingilia kesi za madai, kama wanakiuka taratibu zozote waitwe mahakamani kwa wito maalumu na sio kuvamiwa na kupigwa.
Heche amesema kesi ya Chadema ni ya madai na aliyezuiwa kufanya shughuli za kisiasa ni bodi ya wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema, si viongozi wengine wala wanachama.