Mwanamuziki wa Bongo Fleva Rayvanny (Raymond Mwakyusa) anatarajiwa kutumbuiza kwenye hafla ya ufunguzi wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), inayotarajiwa kuanza Agosti 2, 2025.
Kutokana na tukio hilo la kihistoria maandalizi ya mechi ya ufunguzi ya mashindano hayo itakayopigwa Uwanja wa Mkapa kati ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, na Burkina Faso, yanazidi kupamba moto ambapo kutakuwa na burudani mbalimbali ikiwemo burudani itakayotolewa na msanii huyo.
Mbali na mechi hiyo timu ya taifa ya Madagascar inatarajiwa kuwasili leo Julai 28,2025, ikiwa kundi moja na Stars.
Akizungumza jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alithibitisha kuwa Tanzania iko tayari kikamilifu kuandaa mechi za Kundi B na D.
Mechi zote za kundi hilo zitachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, huku zile za Kundi D zikipigwa Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan.
“Maandalizi yanaendelea kupamba moto,” alisema Msigwa. “Leo tunawakaribisha wachezaji wa timu ya taifa ya Madagascar.
Baadhi ya wachezaji wa Taifa Stars waliokuwa Arusha kwa ajili ya mashindano maalum nao watawasili Dar es Salaam leo, huku wengine wakitarajiwa kufika kesho.”
Aliongeza kuwa maofisa kutoka Mauritania pia watawasili leo, na timu yao inatarajiwa kufika muda mfupi baadaye. Jamhuri ya Afrika ya Kati inakamilisha orodha ya timu za Kundi B zitakazoshiriki mechi za Dar es Salaam.
Kwa upande wa Zanzibar, maandalizi yamekamilika kwa kiwango cha juu. Msigwa alisema kuwa vigogo wa Kundi D, Senegal na Nigeria tayari wamewasili na wanaendelea kujiweka sawa visiwani humo, huku Sudan na Congo Brazzaville wakitarajiwa kuwasili siku chache zijazo.
“Ushirikiano kati ya serikali, waandaaji, na mashirikisho ya soka ya kanda umeonyesha mafanikio makubwa. Kila kitu kiko tayari kwa mashindano ya mafanikiona tunatarajia msanii Rayvanny atatumbuiza siku ya ufunguzi,” alisisitiza.
CHAN 2024, inatarajiwa kuvutia watazamaji wengi wa ndani na nje ya nchi, na kuonyesha uwezo wa Tanzania na Zanzibar kuandaa mashindano makubwa ya soka barani Afrika.
Pia mashindano haya yanatoa fursa ya kipekee kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani barani Afrika kuonyesha vipaji vyao na kutambulika kimataifa.
Zikiwa zimesalia siku chache, mashabiki wa soka nchini Tanzania wanasubiri kwa shauku kubwa kuwapa sapoti Taifa Stars katika mechi hiyo muhimu ya ufunguzi dhidi ya Burkina Faso.