Wanandoa wakutwa wamefariki ndani ya nyumba yao

Rungwe. Vilio, simanzi, taharuki na sintofahamu vimetawala katika kitongoji na kijiji cha Isajilo kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya kufuatia vifo vya wanandoa, Huruma Mwakanyamale na mumewe, Richard Mwaluko, wakutwa wamefia ndani.

Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia Jumamosi Julai 26, 2025 kwenye kitongoji cha Katumba, kijiji cha Mpuguso, huku familia ya Huruma ikishangazwa na tukio hilo, kwani wenza hao hawakuwahi kuripoti mgogoro.

Mwananchi lililofika Kitongoji cha Katumba yalikofanyika mazishi ya Huruma, lilizungumza na Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Emmanuel Mwandembwa aliyethibitisha  kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa wamepokea kwa mshtuko mauaji hayo. 

Amesema aligundua tukio hilo saa 7 mchana Jumamosi baada ya kupokea taarifa kutoka kwa balozi wa mtaa wa Fifty walipokuwa wakiishi na wanandoa hao, huku milango ya nyumba ikiwa imefungwa. 

Anaongeza kuwa baada ya kufika na kukuta milango imefungwa aliamua kutoa maturubai kwenye dirisha na kuchungulia chumbani na kuona Richard ananing’inia kwenye dali na kamba shingoni. 

“Nilimpitisha mtoto mmoja dirishani, akafungua milango, nikaingia, nikamuona mwanaume amejifunga kamba amefariki, baadaye mtoto huyo akaniambia na mama haamki, nikaingia kitandani, nikafunua nikaona mwanamke naye amechomwa visu vingi shingoni na amefariki.”

“Hili ni tukio la kwanza katika kitongoji changu tangu nianze kuwa mwenyekiti 2009, imetushtua sana na zipo hatua tutachukua kama serikali ya mtaa kuona tunakomeshaje yasijitokeze tena,”amesema Mwandembwa. 

Amewataka wananchi kutojichukulia sheria mkononi badala yake inapotokea tatizo zifahamishwe mamlaka ili zishughulike nayo, na kuwaomba familia zilizopoteza ndugu zao kuwa na uvumilivu. 

Ameongeza kuwa mkakati walionao ni kuitisha mkutano wa dharura utakaohusisha wananchi ili wazungumzie usalama wa watu kuanzia ngazi za familia ili kuondokana na vitendo hivyo vya mauaji. 

Familia ya marehemu yasimulia

Vaileth Mwakanyamale ambaye ni dada wa marehemu Huruma, akizungumzia tukio hilo kwenye mazishi hayo amesema hadi tukio hilo linatokea, hawakuwahi kupata taarifa za mgogoro baina ya wawili hao. 

Amesema kama familia bado wanasubiri msimamo wa wazazi kwa kuwa watoto wote wanajitegemea na kila mmoja alikuwa na familia yake. 

“Hatujui ni nini kimewakuta kwa kuwa wamekuwa katika mahusiano kwa miaka sita na wamefanikiwa kupata mtoto mmoja wa miaka mitano, nashindwa nielezeje lakini msimamo upo kwa wazazi wetu kwa kuwa wote wapo,” amesema Vaileth.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Salensi Mwakanyamale amesema ukoo wa Mwakanyamale ni mdogo akitoa shukurani kwa waliofika kumuaga marehemu na serikali iliyofika kuweka ulinzi na usalama pamoja na viongozi wa dini. 

“Huruma hajaugua, maneno ni magumu sana mimi niseme ameuawa, hakuwahi kuja nyumbani inaumiza sana mioyo yetu na tunamuachia Mungu, amepanga njia yake, hapa katika familia alikuwa kiungo.

“Baba mdogo aliniita, alikuwa na upendo kwa watu wengi, ukifika pale Katumba alikuwa na uchangamfu kwa kila mtu, tumeumia na kusikitika,” amesema Mwakanyamale. 

Katekista Edward Mwasalwiba aliyeshiriki maziko hayo amesema ni masikitiko kuachwa na mpendwa wao akiiomba jamii kuendelea kujikita kuabudu na kumtukuza Mungu ili matukio hayo yasitokee tena. 

Amesema marehemu hakutarajia kumkuta yaliyomkuta kwa kuwa hata ndugu, jamaa na marafiki hawakuweza kumuuguza, akilaani matukio ya mauaji. 

“Tumpende Mungu na kumuabudu yeye ili tuweze kuwa salama, lakini tuishi kwa mapenzi na familia zetu, inapotokea tatizo tusemezane, hatujui siku wala saa yetu ya kuondoka,” amesema mtumishi huyo wa kiroho. 

Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Antony Mkwama amesema hana taarifa na kuahidi kufuatilia kisha kutoa taarifa.

“Sina taarifa kuhusiana na tukio hilo, nitafuatilia kwa kina nijue nini kilitokea kisha nitatoa taarifa.”