Mchujo watiania CCM ulivyofanyika hadi usiku mnene

Dar es Salaam. Imechukua zaidi ya saa za kawaida za kazi kwa wajumbe wa Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuchuja majina ya watiania wa nafasi za ubunge na uwakilishi.

Makada hao ambao wakivuka michakato ya ndani ya CCM watakwenda kuchuana na vyama vingine katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Kamati hiyo inatekeleza jukumu lake la kusimamia mwenendo wa nidhamu ya wanachama hao waliotiania kuomba ridhaa ya chama hicho, wagombea ubunge na uwakilishi, kisha inapendekeza kwa Kamati Kuu kwa hatua ya uteuzi.

Kikao hicho kilichoanza jana Jumapili Julai 27, kilitamatika saa tisa usiku wa Julai 28, 2025, jambo linalothibitisha uzito wa kazi iliyokuwa inafanywa na wajumbe wa kamati hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan.

Kamati hiyo inaundwa na Rais Samia, Makamu wenyeviti, Stephen Wasira (Bara) na Rais Hussein Ali Mwinyi (Zanzibar).

Pia, kuna Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Katibu Mkuu, John Mongella (Bara) na Dk Mohamed Said Dimwa (Zanzibar). Wajumbe wengine kwa mujibu wa picha mnato zilizotolewa na CCM walikuwamo Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na wajumbe wengine wanne.

Imechukua takriban muongo mmoja, tangu chama hicho kisahau vikao vya kitaifa vinavyotamatika usiku wa manane.

Kilichotokea jana kinakumbusha enzi za CCM ya miaka 10 iliyopita, iliyokuwa na vikao vya uteuzi na vingine vilivyofanyika usiku za mchana.

Inawezekana kuchelewa kwa kikao hicho kumetokana na idadi kubwa ya watiania na pengine wengi wazuri, hivyo inaweka ugumu wa kuamua yupi apitishwe na yupi aachwe, kama inavyoelezwa na Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Ajali Nguyuhambi.

Mwanazuoni huyo, amesema kwa upande mwingine, pengine watiania wengi ni wale waliojitokeza kuonesha sura zao, lakini hawana dhamira ya dhati ya kuwa wabunge au wawakilishi, hivyo kamati inaongeza umakini isikosee kuwapitisha.

Hivi karibuni, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla alisema zaidi ya makada 10,000 wamejitokeza kuomba nafasi ya ubunge na uwakilishi.

Sababu nyingine ya kuchukua muda kwa kikao hicho, alisema ni uhalisia wa vitendo vya uvunjifu wa maadili vilivyosikika mara kadhaa, na kwa kuwa kamati hiyo ndiyo inayohusika na kufuatilia hilo, kikao chake kimechukua muda kuchuja kila mmoja.

Hata hivyo, Dk Nguyuhambi amesema kumalizika usiku wa manane kwa kikao hicho, kunaashiria vikao vya ngazi za chini havikuwa na umakini wa kutosha kiasi cha kuvisaidia vya juu kufanya uamuazi kwa urahisi.

“Mwisho wa siku ni kutafuta wagombea ambao chama kinadhani hakitaangushwa,” amesema Dk Nguyuhambi.

Kihistoria vikao vya kitaifa vya CCM vilivyochukua saa nyingi ni vile vilivyohusisha mchakato wa kuwapata wagombea wa urais, sio ubunge na uwakilishi kama ilivyo sasa.

Hiyo ilishuhudiwa katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995. Kati ya wagombea waliotajwa kuwania urais kupitia chama hicho ni Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Kingunge Ngombale-Mwiru, Joseph Warioba na wengineo.

Vikao vya Kamati Kuu vilivyofanyika Dodoma vilidumu hadi saa tisa usiku wa manane.

Iliripotiwa mvutano ulikuwa mkubwa, hasa kati ya kambi ya Mkapa na Kikwete. Lakini hatimaye, Mkapa alipitishwa kuwa mgombea wa CCM na kuwa Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania.

Julai 2005, wakati CCM ikijiandaa kumchagua mgombea urais kuchukua nafasi ya Mkapa aliyemaliza muda wake, vikao vilidumu hadi alfajiri. Wagombea walikuwa 11, miongoni mwao Jakaya Kikwete, Salim Ahmed Salim, Mark Mwandosya na Anna Tibaijuka.

Mchakato wa kuwachuja hadi kubakia watatu ulifanyika hadi saa tisa usiku na baadaye Kamati Kuu ilimpendekeza Kikwete.

 Hicho kilikuwa moja ya vikao virefu zaidi kuwahi kufanyika ndani ya CCM.

Hali kama hiyo, ilijirudia Julai 2015, katika kikao kilichovuta hisia za wengi.

Jina la John Magufuli lilitangazwa kuwa mgombea urais kupitia CCM, akiwashinda vigogo kama Edward Lowassa, Bernard Membe na Asha-Rose Migiro.

Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya vikao virefu vilivyoanza asubuhi na kudumu hadi saa nane usiku.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa Kamati Kuu ilikaa kwa zaidi ya saa 18 na baadhi ya wajumbe walilala kwa zamu nje ya ukumbi wa mikutano.

Akizungumzia hilo, mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu, amesema vikao vinavyovuka mchana mara nyingi vinahusisha uamuzi mgumu.

Mathalan, Kamati ya Usalama na Maadili, amesema ni kikao kinachogusa kila fomu ya mgombea, kufuatilia mwenendo wake ndani na nje ya chama kabla ya kuamua.

Katika kikao hicho, ameeleza kuna wajumbe wanajua taarifa zaidi ya zile zinazojulikana kuhusu muhusika, hali inayosababisha mabishano.

“Kuna wakati mjumbe atasema mtiania ana shida fulani anaijua ataombwa ushahidi wakati mwingine anauleta. Kwa sababu ushahidi umeletwa kikao kinajiridhisha na mtiania anakatwa, hayo mambo yanachukua muda,” ameeleza.

Hata hivyo, kikao hicho cha kamati ya usalama na maadili, kimefanyika wakati ambao awali hakikuwa katika mpango wa chama hicho, lakini mabadiliko ya ratiba yakakiingiza kwenye kalenda.

Mmoja wa kigogo mwandamizi wa chama hicho ambaye ameomba hifadhi ya jina lake aliyezungumza na Mwananchi juzi kuhusu mchakato huo amesema: “Hii wiki ni ngumu kwelikweli, tunapaswa kusimamia kwa weledi na umakini mkubwa ili tupate wagombea wazuri.”

“Humu ndio tutapata mameya, wenyeviti wa halmashauri, lakini kupitia wabunge na wawakilishi ndio marais wetu (wa Tanzania na Zanzibar) watateua mawaziri na manaibu wao. Kwa hiyo tuko makini kwelikweli kuhakikisha tunapata watu sahihi.”