SERIKALI YAJIZATITI MAPAMBANO HOMA YA INI WANACHI WATAKIWA KUJITOKEZA KUPATA CHANJO


::::::::::

Na WAF – Songea, RUVUMA

Wananchi kote nchini wametakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya homa ya ini ikiwa ni pamoja na kupata chanjo dhidi ya ugonjwa wa homa hiyo, huku akisisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania imeweka nguvu kubwa kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama Julai 28, 2025 alipokuwa akitoa tamko la Siku ya Homa ya Ini Duniani kwa wananchi kupitia vyombo vya habari mkoani Ruvuma

“Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na juhudi za utoaji wa huduma tiba na kinga dhidi ya Homa ya Ini, hivi sasa huduma za upimaji na matibabu zinatolewa kwenye Hospitali zote za Rufaa za Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili” amesema Waziri Mhagama.

Amebainisha kuwa vituo vya huduma za afya kuanzia ngazi ya Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati vitaendelea na utaratibu wa kupima Homa ya Ini na kutoa rufaa kwa huduma za Homa ya hiyo, huku mipango ya Serikali ikiendelea kuviwezesha vituo hivyo kutoa huduma kamili.

Waziri Mhagama amesema takwimu za utafi wa UKIMWI (THIS 2022/2023) zinaonyesha kuwa hali ya ushamiri wa Homa ya Ini ni 3.5%, kwa Homa ya Ini inayosababishwa na virusi aina ya B na 0.2% kwa virusi homa ya ini inayosababishwa na aina ya virusi C ikiwa imeshuka kutoka takwimu za utafiti wa UKIMWI (THIS 2016/17) ilipokua asilimia 4. kwa Homa ya Ini inayoambukizwa na virusi aina B na asilimia moja kwa Homa ya Ini inayoambukizwa virusi aina C.

Amebainisha kuwa kupungua kwa maambukizi ya Homa ya ini ni juhudi za pamoja kati ya Serikali na Wadau wa Sekta ya Afya waliokwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo wakiwa na lengo la kidunia la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo 2030.

“Hapa nchini Serikali inatoa huduma za chanjo ya Homa ya Ini aina ya B bila malipo yoyote kwa watoto wachanga na chanjo ya Homa ya Ini aina B kwa watu wazima inatolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa utaratibu wa kuchangia gharama kiasi” amesema Waziri Mhagama na kufafanua kuwa chanjo hiyo ilianza kutolewa kwa watoto nchini waliozaliwa kuanzia Mwaka 2002 kwani ni moj ya chanjo ilipo kwenye mchanganyiko wa chanjo za magonjwa matano kwa chanjo moja (Pentavalent).

Homa ya Ini husababishwa na virusi ambavyo vipo katika makundi matano, yaani A, B, C, D na E. 

Aina ya virusi vya A na E huambukizwa kwa njia ya kunywa maji na chakula kisichokuwa salama kwa kuchafuliwa na kinyesi chenye maambukizi ya virusi hivyo ambazo dalili zinafanana kwa kiasi kikubwa na uambukizwaji wa magonjwa ya kuhara.

 Virusi aina ya B, C na D huambukizwa kwa njia sawa na za magonjwa ya ngono na VVU/UKIMWI kama kuongezewa damu yenye virusi vya ugonjwa huo, kujamiiana, utumiaji usio salama wa sindano na kujichoma na vitu vyenye ncha kali, majimaji ya mgonjwa kumpata mtu mwingine kama ana kidonda, na pia mama anaweza kumwambukiza mtoto wake wakati wa kujifungua.

 Aina ya homa ya Ini inayosababishwa na virusi vya kundi B ndiyo inayoongoza kwa maambukizi nchini.