Dar es Salaam. Mbunge wa Bumbuli mkoani Tanga anayemaliza muda wake, January Makamba hajateuliwa kuwania nafasi hiyo baada ya jina lake kushindwa kupenya kwenye mchujo uliofanywa na Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amewataja wagombea sita watakaochuana ni Hidaya Kilima, Zahoro Hanuna, Ramadhan Singano, Rashid Kiula, Silas Shehemba na John Kilima.
Makamba, ambaye amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri kuanzia Serikali ya awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete, ya tano iliyoongozwa na hayati John Magufuli hadi sita ya Samia Suluhu Hassan, jina lake limekatwa.
Makamba ambaye amebobea katika uchambuzi na usuluhishi wa migogoro aliingia bungeni kuanzia mwaka 2010, amewahi kuwa msaidizi wa Rais wa awamu nne, Jakaya Kikwete kuanzia mwaka 2005 hadi 2010.
Wakati anawania Jimbo la Bumbuli, Makamba alishinda kwa kupata kura 14,612 dhidi ya mpinzani wake William Sherukindo aliyepata 1,700 ambaye pia alikuwa akitetea jimbo hilo kwa awamu nyingine.
Amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, chini ya utawala wa Kikwete, mwaka 2012, kisha mwaka 2016 akawa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), kabla ya uteuzi wake kutenguliwa na hayati Magufuli mwaka 2019.
Akiwa Waziri Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Makamba alikuwa chini ya Rais Samia (wakati huo akiwa Makamu wa Rais) ambapo walifanya kazi kwa ukaribu na mbunge huyo.
Mwaka 2021, Rais wa awamu ya sita, Samia alimteua Makamba kuwa Waziri wa Nishati, baadaye akamuhamisha kwenda Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Utenguzi huo wa Makamba, ulikwenda sambamba na Nape Nnauye aliyekuwa Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari, ambaye pia ni mbunge wa Mtama mkoani Lindi.
Hata hivyo, Julai mwaka 2024, Rais Samia alitengua uteuzi wa Makamba katika taarifa hiyo, mamlaka husika haikuweka wazi sababu za kumtengua mwanasiasa huyo.
Februari 24, 2025, akiwa ziara ya kikazi mkoani Tanga, Rais Samia alitangaza kumrudisha Makamba baada ya kile alichodai alimpiga kofi.
Mkuu huyo wa nchi, alieleza hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Lushoto ambapo alimkumbatia mbunge huyo, akieleza kwa mfano wa kifamilia jinsi alivyosimamia uhusiano wao.
Katika mkutano akiwa mwisho kumaliza hotuba yake, Rais Samia alisema:”Lakini mwisho kabisa nataka nimuite mwanangu January hapa aje huku, arudi kwa mama. Sisi wamama mnatujua, ukimkera mama anakupiga kofi, anakufichia chakula si ndio hivyo.”
“Sasa mwanangu nilimpiga kofi, nikamfichia chakula, lakini leo namrudisha kwa mama. Haya mwanangu njoo,” alisema Rais Samia huku akimkumbatia Makamba.