WAKATI Yanga ikiendelea na mchakato wa kujiimarisha kwa ajili ya msimu ujao wa 2025-2026,kuna mafundi sita wameshushwa kuunda benchi jipya la ufundi litakaloongozwa na Mfaransa, Romain Folz.
Folz ambaye amekuwa mtu wa kwanza kutambulishwa katika benchi hilo akichukua nafasi ya Miloud Hamdi, ana kazi kubwa ya kuhakikisha msimu ujao timu hiyo inafika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, pia kutetea mataji yote iliyoshinda Yanga msimu uliopita 2024-2025 ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Kombe la Muungano na Kombe la FA. Bila ya kusahau kufanya vizuri katika mechi za maandalizi ambapo Yanga ilibeba Kombe la Toyota ilipoalikwa nchini Afrika Kusini.
Ni Romain Folz. Raia huyo wa Ufaransa, si mgeni katika soka la Afrika kwani katika umri wake wa miaka 35, amefundisha timu za Bechem United na Ashanti Gold zote za Ghana, Pyramids (Misri) ambapo alikuwa kocha msaidizi na mtaalamu wa kufuatilia viwango vya wachezaji.
Zingine ni Township Rollers (Botswana), Horoya (Guinea), Marumo Gallants na Amazulu FC za Afrika Kusini na Mamelodi Sundows ya nchini humo akiwa kocha msaidizi.
Amefanya kazi katika kikosi cha Olimpique Akbou (Algeria) na Chamois Niortais FC ya Ufaransa. Pia amefanya kazi katika Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) akiwa mtaalamu wa ufundi.
Folz atasaidiwa na Manu RodrÃguez raia wa Hispania mwenye umri wa miaka 33 ambapo huyu pia amebobea katika kuwania washambuliaji.
RodrÃguez na Folz wanakutana tena ndani ya Yanga kwani huko nyuma wamefanya kazi pamoja kwenye timu kadhaa ikiwemo Virginia Alliance (Marekani) na Ashanti Gold (Ghana).
Rekodi zinaonesha mwaka 2013 hadi 2016, alikuwa kocha wa timu mbalimbali za vijana za Hispania, kisha 2018 akawa kocha msaidizi katika kikosi cha West Virginia Alliance wakati kocha mkuu akiwa Romain Folz.
Mwaka 2018 hadi 2019 alikuwa kocha wa Juventud Canadiense ya Guatemala. Mwaka 2021 alifanya kazi na Romain Folz katika kikosi cha Ashanti Gold ya Ghana.
Kuanzia 2022 hadi 2024, akafanya kazi na FIFA akiwa ni Mtaalamu wa Maendeleo katika kukuza vipaji akifanya kazi kwa ukaribu na nchi za Costa Rica na Venezuela.
Baada ya hapo, Januari 2025 akateuliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Costa Rica akihusika pia kwenye timu za vijana za chini ya miaka 17, 20 na 23.
Pia Kocha Manu Rodriguez amefanya kazi kwa ukaribu na klabu kubwa Ulaya ikiwemo Real Madrid ya Hispania na Olympique Lyon ya Ufaransa akiwa kama mtaalamu wa mafunzo ya ushambuliaji.
Majdi Ben Mansour Mnasria ndiye atakuwa kocha wa makipa akichukua rasmi nafasi ya Alaa Meskini ambaye aliondoka Februari mwaka huu akitua FAR Rabat ya Morocco. Wakati Meskini akiwa ameondoka, kocha wa makipa wa Yanga alikuwa Soud Slim ambaye awali alikuwa katika benchi la ufundi la timu ya vijana klabuni hapo.
Kocha Mnasria raia wa Tunisia aliyezaliwa Juni 13, 1976, kwa sasa ana umri wa miaka 49 akiwa pia amewahi kufanya kazi na Folz kwenye kikosi cha Olympique Akbou kinachoshiriki Ligi Kuu ya Algeria na Lamontville Golden Arrows ya Afrika Kusini.
Kocha huyo ana uezofu mkubwa akiwa amefundisha katika nchi za Tunisia, Algeria na Afrika Kusini, akifanya kazi na klabu mbalimbali zikiwemo El Gawafel Sportives de Gafsa, Stade Gabsien Sports, Averine Sportif de Casserine na Tunisia ES Metlaoui.
MCHAMBUZI WA VIDEO
Katika kitengo cha mtaalamu wa uchambuzi wa mikanda ya video (video analyst), kuna Thulani Thekiso raia wa Afrika Kusini ambaye amechukua nafasi ya Msauzi mwenzake, Mpho Maruping, aliyeripotiwa kumfuata Sead Ramovic ambaye anaionoa CR Belouzdad ya Algeria baada ya kuondoka Yanga.
Chyna Tshephang Mokaila ndiye amepewa jukumu la kuwa kocha wa viungo ndani ya kikosi cha Yanga akichukua nafasi ya Taibi Lagrouni raia wa Morocco.
Mokaila raia wa Afrika Kusini, katika safari yake kabla ya kutua Yanga, amepitia klabu mbalimbali ikiwemo Township Rollers ya Botswana, Marumo Gallants (Afrika Kusini), Amazulu (Afrika Kusini), Horoya AC (Guinea), Al Ahli Tripoli (Libya) na Timu ya Taifa ya Botswana iliyofuzu Afcon 2025.
Katika nafasi hii, Paul Matthews raia wa Afrika Kusini ndiye amekabidhiwa kijiti hiki kilichoachwa na Abdihamid Moallin ambaye naye anatajwa kwenda kuungana na Sead Ramovic.
Mathwes ni mzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika majukumu hayo sambamba na ufundishaji, skauti, uchambuzi na usimamizi wa timu.
Rekodi zinaonesha kutokana na uzoefu huo, amekuwa mtu muhimu katika benchi la ufundi kila alipopita akisaidia makocha wakuu na timu kucheza kwa kiwango cha juu, kuwachambua wapinzani na kuchambua ubora wa mchezaji mmoja mmoja.
Pia ni kiongozi anayeaminika akiwa amedhihirisha hilo nchini Afrika Kusini alipopewa jukumu la kuwa skauti mkuu wa kusaka vipaji.
Timu alizowahi kufanya nazo kazi kabla ya kutua Yanga ni Supersport United, University of Pretoria FC, Thanda Royal Zulu FC, Tembisa Classic FC na Jomo Cosmos zote za Afrika Kusini.
Ujio wa mafundi hao sita, unaashiria kwamba Yanga ipo tayari kwa kuanza maandalizi ya msimu ujao 2025-2026 ambapo Agosti 13 mwaka huu kikosi hicho kinakwenda Rwanda baada ya kupewa mualiko maalum na wenyeji wao Rayon Sport watakaocheza nao mchezo wa kirafiki Agosti 15.
Baada ya mchezo huo, Mwanaspoti linafahamu Yanga itaanza safari ya kwenda kambini Misri kujiandaa na msimu mpya.