SIMBA wameonyesha ukubwa wao kwa mara nyingine. Kuna jambo ambalo wamefanya kwenye kambi ya timu ya Taifa ya Kenya Harambee Stars ambalo limemtibua Kocha Benni McCarthy.
Ni jinsi walivyoufanya kibabe usajili wa mshambuliaji wao mpya, Mohammed Bajaber na kuumaliza kwa haraka bila kumpa hata nafasi ya kumeza mate.
Simba imeendelea kuboresha kikosi chake kwa kusajili wachezaji kadhaa wakubwa imekamilisha dili ya staa huyo ambaye alikuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Kenya kinachojiandaa na Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (CHAN 2024).
Awali ilielezwa kuwa timu kadhaa za Tanzania ikiwemo Yanga na Azam FC zilikuwa zikimtaka mchezaji huyo ambaye alionyesha kiwango bora kwenye ligi ya Kenya, lakini Simba ndiyo imefanikiwa kuwahi dili hilo na kumuondoa rasmi kwenye CHAN 2024.
Chanzo cha uhakika kimeliambia Mwanaspoti kuwa mshambuliaji huyo ambaye alikuwa akiitumikia Police ya Kenya msimu uliopita na kufunga mabao tisa kwenye ligi aliondoka kambini juzi na kutua Dar es Salaam ambapo ameshasaini mkataba wa miaka miwili na Simba na anaondoka kwenda kambini Misri.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kulikuwa na mazungumzo ya awali, yakimtaka staa huyo mwenye miaka 22 asisaini kwanza Simba hadi michuano ya CHAN 2024, itakapomalizika ili awe na uhakika wa kuitumikia Kenya kwenye michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wa ndani pekee, lakini hilo lilishindikana baada ya Simba kumtaka mchezaji wao kutua nchini haraka bila mazungumzo yoyote.
Habari zinasema kwamba Simba walishtukia kwamba endapo wakimuacha mchezaji huyo akicheza japo mechi mbili za CHAN mawakala wa nje wanaweza kupanda dau Msimbazi wakabaki kwenye mataa, hivyo wakaamua kumaliza jambo kwa haraka.
“Kulikuwa na mazungumzo awali Simba wakiombwa wamsubiri mchezaji huyo hadi hapo michuano ya CHAN itakapomalizika ndiyo wamsajili kwa kuwa akishasaini mkataba nje ya Kenya hana ruhusa tena ya kucheza CHAN, walihakikishiwa kuwa atalindwa.
Kenya tayari imepata pigo kubwa kwa wachezaji wake kuondoka kambini, lakini Simba nao walihofia wanaweza kuzidiwa ujanja kwa kuwa ni mchezaji ambaye alitakiwa hata na watani wao wa jadi, Yanga hivyo walihofia wanaweza kuzidiwa ujanja.
“Hata hivyo, Simba waligoma na kumtaka mchezaji wao, unajua ni hatari wakati mwingine kama umemweka kwenye listi yako, ukimuacha akicheza mechi mbili hivi anaweza kuonekana bora na timu nyingine zikamshawishi, hivyo walivyokubaliana, walimtaka kwa ajili ya kusaini mkataba, kupiga picha na kujiandaa na maandalizi ya msimu mpya,” kilisema chanzo kutoka ndani ya kikosi hicho.
Hata hivyo, kuondoka kwa mchezaji huyo ambaye amewahi kufanya majaribio kwenye kikosi cha Midtjylland cha Denmark hili ni pigo kubwa kwa Kenya ambayo kwa sasa imeshawapoteza wachezaji watano tangu ilipoanza kambi ya kujiandaa na michuano hii ya CHAN baada ya kusaini mikataba na timu za nje ya Kenya.
Awali mshambuliaji wa zamani wa Kakamega Homeboyz Moses Shummah na Emmanuel Osoro wa Talanta FC waliondoka kambini baada ya kwenda Zambia kujiunga na Power Dynamos.
Pia timu hiyo imewaondoa mastaa wawili Marvin Nabwire na Brian Musa ambao walipata majeraha kwenye mchezo wa kirafiki wikiendi iliyopita na tayari kocha ameshawaita Edward Omondi wa Sofapaka na Crispine Erambo wa Tusker kuziba nafasi zao.
Bajaber alikuwa anapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye michuano hii na alikuwa anatajwa kuwa mmoja kati ya wachezaji wanaopendwa zaidi na kocha Benni McCarthy, akiwa aliisaidia Police kutwaa ubingwa wa Kenya kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo, akiwa ana uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa mwisho, winga wa kulia na kushoto.
Staa huyo ambaye alifunga kwenye mchezo wake wa kwanza wa timu ya Taifa dhidi ya Gambia, ameshaitumikia Kenya kwenye michezo miwili tu akiwa na bao moja.
Tayari kocha huyo raia wa Afrika Kusini ameshamuita kikosini nyota wa Shabana Brian Michira, ambaye alichezea Tore Bobe.
Kenya ambayo ni moja kati ya nchi zinazoandaa michuano hii ipo Kundi A ambapo itacheza na vigogo Congo (DRC) Jumapili Agosti 3, 2025. Kundi hilo likiwa pia na timu za Morocco, Angola, na Zambia.