Simba Queens yasajili kipa Mganda

SIMBA Queens inaendelea kushusha vyuma kimyakimya kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano ya Ligi Kuu na inaelezwa imemalizana na kipa Mganda Ruth Aturo.

Simba Queens iliwapa mkono wa kwaheri makipa wawili Carolyne Rufaa, aliyekuwa nje ya uwanja kwa msimu mzima akiuguza majeraha na Gelwa Yona. Klabu hiyo inaendelea na Janet Shija na Winfrida Ceda.

Akizungumza na Mwanaspoti, wakala wa mchezaji huyo ambaye aliitumikia Tausi ya Tanzania kwa mwezi mmoja, Amosi Mlandali, alisema tayari dili hilo limekamilika na kwa sasa ni mchezaji halali wa Simba Queens.

“Tayari amesaini mkataba wa miaka miwili, kwa hiyo msimu ujao mtamuona Msimbazi. Walivunja mkataba na Tausi na kumnunua moja kwa moja,” alisema.

Mbali na Aturo, Simba Queens pia imekamilisha usajili wa mshambuliaji raia wa Kenya, Cynthia Musungu akitokea Besiktas ya Uturuki.

“Ni kweli pia Musungu namsimamia na yeye amesaini mkataba wa miaka miwili baada ya kumalizana na Besiktas ya Uturuki. Kilichobaki ni kwa timu kuanza kambi rasmi mwanzoni mwa mwezi ujao.”

Aturo aliisaidia Tausi FC, iliyopanda daraja msimu huu, kunyakua ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza akiwa kipa pekee aliyeruhusu mabao machache.

Aturo ni miongoni mwa makipa wenye uzoefu kimataifa hivyo anaweza kuisaidia Simba msimu ujao ambao imepanga kuanza upya. Mbali na kuwa kiongozi uwanjani, ni golikipa anayejua kucheza mipira ya juu, kwa miguu, na mzuri wa kuanzisha mashambulizi kutokea chini. Hii ni mara yake ya kwanza kucheza Tanzania, na ndani ya muda mfupi aliisaidia Tausi kupanda daraja. Aliwahi kupita klabu kama Kawempe Muslim na UCU Lady Cardinals za Uganda, FC KTP ya Finland, Al Shabab na Altaqadum za Saudia Arabia pamoja na Vihiga Queens ya Kenya.

Ndiye kipa namba moja wa timu ya taifa ya Uganda na amekuwa na mafanikio ikiwemo kuchukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike Uganda (2018).