Uzoefu wa Vijana Queens kwenye Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kwa wanawake (WBDL), ndiyo ulioibeba katika mchezo wake na Ukonga Queens.
Katika mchezo huo uliopigwa Donbosco, Upanga, timu ya Vijana Queens ilishinda kwa pointi 59-47 ikiwatumia wachezaji iliowapandisha kutoka kikosi cha pili cha City Queens ambapo ilianza kuongoza katika robo ya kwanza kwa pointi 21-10, 15-11, 22-8, 14-5.
Katika mchezo huo Salma Sandali aliongoza kwa kufunga pointi 16 ilhali upande wa Ukonga Queens alikuwa Magreth Kihonda aliyetupia 11. Katika mchezo mwingine Jeshi Stars ilidhihirisha ubora baada ya kuifunga DB Lioness kwa pointi 60-51.
Jeshi Stars iliingia uwanjani kwa tahadhari ikihofia kupoteza mchezo kutokana na DB Lioness kuwa na nyota anayejua kucheka na nyavu, Taudencia Katumbi.
Taudencia ambaye ni raia wa Kenya, ni mmoja wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kufunga pointi.
Kwa upande wa DB Lioness kilichofanya ikapoteza mchezo ni kutokana na wachezaji kumtegemea nyota huyo kufunga ilhali wengine wakiwa na uwezo wa kutupia. Jeshi Stars ilimdhibiti mchezaji huyo kupitia kwa Anamary Cyprian ambaye alitembea naye kila alipokuwa uwanjani, hivyo kushindwa kufanya lolote.