Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), imefikia patamu kutokana na timu kupambana kusaka nafasi ya kucheza hatua ya robo fainali.
Ukiondoa timu za Dar City yenye pointi 24, Pazi 22, Stein Warriors 21 na JKT 21 zilizojiweka katika mazingira mazuri ya kucheza hatua hiyo, timu zinazopambana kutafuta nafasi nne za kucheza robo fainali ni DB Oratory yenye pointi 19, Srelio (18), Vijana (18), ABC (16), Savio (14), KIUT (15) na UDSM Outsiders (15).
Kutokana na hali hiyo baadhi ya mashabiki wanaohudhuria mechi za ligi katika Uwanja wa Donbosco, Upanga walisema michuano hiyo imekuwa ikiongezeka ubora na kinachotarajiwa kutokea mwaka huu huenda kikaziacha midomo wazi baadhi ya timu zilizozowea kutinga hatua hiyo.
“Ingawa inaweza kuwa gumu, lakini inawezekana tukashuhudia wakali fulani wakishindwa kutinga robo fainali maana kila kunapokucha kunakuja na maajabu yake,” alisema Aisha Mjojoli, shabiki wa Savio.
Naye Idris Joheri alisema kuna uwezekano mkubwa baadhi ya wachezaji wenye majina makubwa wakaishia kushuhudia robo fainali wakiwa majukwaani kama watazamaji kwa sababu ushindani ni mkubwa kati ya timu na timu na hivyo kutinga hatua hiyo itakuwa ni kazi ngumu.
“Unapotazama kila mchezo unaona kabisa kwamba vita ni kubwa. Nadhani wakongwe ili wafuzu inabidi wapambane kwelikweli wasije wakaishia kudhalilika,” alisema Joheri.