Kinachotarajiwa kujiri leo kesi ya uhaini ya Lissu

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo Jumatano, Julai 30, 2025 tena anapanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Dar es Salaam, inayoketi Kisutu huku Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) akitarajiwa kutoa hatima uhamishwaji wa kesi hiyo kwenda Mahakama Kuu.

Kesi hiyo imefunguliwa mahakamani hapo kwa ajili ya uchunguzi wa awali kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndio ina mamlaka ya kusikiliza kesi kubwa kama hiyo ya uhaini, baada ya taratibu za msingi kukamilika ukiwemo upelelezi.

Julai 15, 2025 upande wa mashtaka uliiarifu Mahakama hiyo kuwa tayari upelelezi umeshakamilika na kwamba DPP ameridhika na ushahidi uliopo kuwa unatosha kesi hiyo kupelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kuanza usikilizwaji kamili.

“Baada ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) na DPP kusoma jalada hili ameridhika kuwa ushahidi uliopo unajitosheleza kwenda kupeleka kesi Mahakama Kuu,” alisema kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga.

Kutokana na taarifa hiyo kuwasilisha Mahakama Kuu taarifa za kesi hiyo (hati ya mashtaka), kwa ajili ya kuisajili kesi hiyo

Hata hivyo, Wakili Katuga aliieleza mahakama hiyo kuwa wamefungua shauri la maombi madogo Mahakama Kuu.

Wakili Katuga alieleza katika shauri hilo la maombi ya jinai ya mwaka 2025 wanaomba amri ya ulinzi wa baadhi ya mashahidi wanaotarajiwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo, yaani kutowekwa wazi kwa taarifa zao zinaweza kufanya utambulisho wao kubainika.

Alifafanua shauri hilo limefunguliwa chini ya kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023, kinaruhusu kuwasilishwa maombi ya ulinzi wa taarifa za mashahidi kwa ajili ya usalama wao.

Kwa mujibu wa kifungu hicho maombi ya DPP ya ulinzi wa mashahidi husikilizwa na kuamuliwa  upande mmoja.

Hivyo kutokana na kuwepo kwa shauri hilo dogo, Wakili Katuga, chini ya kifungu cha 265 cha CPA aliiomba ahirisho kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa maombi hayo, kabla ya kupeleka kesi hiyo Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Lissu ambaye katika kesi hiyo anajitetea mwenyewe, alipinga  vikali maombi ya Jamhuri ya ahirisho, akidai kuwa baada ya upelelezi kukamilika na DDP kusoma jalada  na kupewa maoni, kilichotakiwa siku hiyo chini ya kifungu cha 262 (6) cha CPA ni kuiarifu Mahakama hiyo kuwa taarifa ya kesi hiyo  imeshapelekwa Mahakama Kuu (kusajili kesi).

Alidai kuwa masharti ya  kifungu hicho hayakuzingatiwa na upande wa mashtaka.

Hivyo aliiomba mahakama kwa kutumia mamlaka yake ya kimahakama ikatae kutoa ahirisho, badala yake iamuru kumfutia mashtaka, aachiwe huru kama mtu asiye na hatia kutoka na mazingira maalumu.

Hata hivyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo anayesikiliza kesi hiyo katika hatua ya awali, Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga alikataa hoja na maombi ya Lissu badala yake akakubaliana na hoja za upande wa mashtaka.

Hakimu Kiswaga alisema kisheria upande wa mashtaka ulikuwa sahihi na Mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kutekeleza kile Lissu alichokiomba.

Hivyo aliahirisha kesi hiyo mpaka leo kwa ajili ya kuangalia kama upande wa mashtaka utakuwa umeshasajili kesi hiyo Mahakama Kuu, ili mahakama hiyo iweze kuendelea na hatua ya uhamishaji wa kesi hiyo.

Kwa hiyo leo upande wa mashtaka unatarajiwa kutoa mwelekeo kama kesi hiyo inahamishwa rasmi kwenda Mahakama Kuu na  imeshasajiliwa huko.

Lakini hilo linategemea hatima ya shauri la maombi ya ulinzi wa mashahidi, kama litakuwa limeshaamuriwa au la.

Kwa hiyo leo Jumatano, kwanza upande wa mashtaka unatarajiwa kutoa mrejesho kama shauri hilo dogo limeshaamuliwa na Mahakama Kuu au la.

Kama litakuwa bado bila shaka Mahakama hiyo haitaweza kuendelea na mwenendo wa uhamishwaji wa kesi hiyo kwenda Mahakama Kuu.

Ikiwa tayari shauri hilo litakuwa limeshaamuliwa upande wa mashtaka utatoa taarifa kama umeshasajili kesi hiyo Mahakama Kuu, jambo ambalo litatoa fursa kwa Mahakama hiyo ya chini kuendelea na hatua ya uhamishwaji wa kesi hiyo kwenda Mahakama Kuu.

Katika hatua hiyo mshtakiwa atasomewa maelezo ya mashahidi wa Jamhuri katika kesi hiyo pamoja na vielelezo vinavyotarajiwa kutumika.

Hapo Mahakama hiyo itakuwa imekamilisha jukumu lake. Hivyo itaamuru kuwa sasa kesi hiyo imehamishwa Mahakama Kuu rasmi na jalada lake litafungwa rasmi mahakamani hapo.

Hivyo mshtakiwa atasubiri wito wa Mahakama Kuu wa kumtaka kufika mahakamani kwa tarehe itakayopangwa kwa ajili ya kuendelea na hatua inayofuata.

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka mola la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, akidaiwa kutenda kosa hili Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam.

Anadaiwa kuwa kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.

Endelea kufuatilia Mwananchi