Dar es Salaam. Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa ujenzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (EACLC) haimaanishi kitakuja kuchukua masoko ya wafanyabiashara wazawa.
Hilo linasemwa baada ya kuwapo kwa kauli zinazotolewa na wadau wakidai kituo hicho huenda kikaua baadhi ya masoko ya ndani, likiwemo lile la Kariakoo kutokana na utendaji kazi wake.
Hayo yamesemwa leo Jumatano, Julai 30, 3035 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya ufunguzi wa kituo hicho unaotarajiwa kufanyika Agosti Mosi 2025 ikiwa ni mabadiliko kutoka Agosti 2 iliyokuwa imetangazwa awali.
Chalamila amesema ujenzi wa kituo hicho ni mfano wa uwekezaji wa ubia ambao Serikali imekuwa ikifanya mara kwa mara katika maeneo tofauti katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati.
“Uwekezaji wa aina hii huwa unafanyika baada ya Serikali kujiridhisha kuwa miradi hiyo itakuwa na tija kwa Watanzania tija ya uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia na kimataifa,” amesema.
Mradi huu wa ACLC uliogharimu zaidi ya Sh282.7 bilioni hadi sasa kimejengwa kwa ubia kati ya wawekezaji kutoka China na Halmashauri ya Ubungo ambao utadumu kwa miaka 32.
Serikali inatarajia kunufaika na mapato ya moja kwa moja ya takriban dola milioni 10 kila mwaka (Sh25.63 bilioni) sambamba na dola 200,000 (Sh512.6 milioni) za ushuru na tozo.
Pia kama nchi inatarajia kuongeza thamani ya biashara ya mauzo ya nje kuwa dola milioni 150 kwa mwaka (Sh384.45 bilioni) ikijumuisha bidhaa zinazoletwa nchini na kupelekwa nchi za jirani, bidhaa za Watanzania zilizouzwa nje kupitia kituo hiki na bidhaa zilizoletwa nchini na kuongezewa thamani kabla ya kuuzwa tena katika masoko ya nje.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila
Chalamila amesema uanzishaji wa kituo hicho unaonyesha dhamira endelevu ya Serikali ya kushirikiana na sekta binafsi katika miradi yenye manufaa kwa Watanzania.
Akitolea mfano wa miradi ya ubia ya namna hiyo ambayo imewahi kutekelezwa miongoni mwake ni uboreshaji wa eneo la zamani la DDC Kariakoo na uanzishwaji wa Mlimani City kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mradi huu ulitekelezwa baada ya kuhamishwa kwa kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo kwenda Mbezi stendi ya Magufuli.
Alieleza Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilihusika katika kumpata mwekezaji wa kuendeleza eneo hilo la zamani, na sasa kuna kituo cha kisasa chenye maduka 2,000 ofisi za kupangisha na eneo kubwa la maegesho.
Kutokana na hilo aliwahamasisha wafanyabiashara wa ndani na wawekezaji wa kigeni kutumia fursa zilizopo za kibiashara.
“Kituo hiki ni mwendelezo wa jitihada zetu za makusudi kukuza uchumi na kuimarisha mazingira rafiki ya biashara,” amesema.
Ripoti zinaonesha kituo hicho chenye zaidi ya maduka 2,000, ofisi, benki, kampuni za usafirishaji, ofisi za forodha na kodi kimeundwa kwa mtindo wa kituo kimoja chenye huduma zote muhimu chini ya paa moja.
Mfumo huu uliounganishwa unawawezesha wafanyabiashara wa Kitanzania kupata urahisi wa kufikia masoko ya China na ya kimataifa, hasa kupitia ununuzi wa jumla na mitandao ya kielektroniki (e-commerce).
Kituo hicho kinatarajiwa kupunguza gharama za uagizaji kwa kuruhusu wafanyabiashara kununua bidhaa moja kwa moja kutoka kwa wauzaji wa jumla wa China hivyo kuokoa muda na fedha za kigeni.
Mmoja wa wafanyabiashara Kariakoo, Geofrey Ndimbo amesema uwepo wa kituo hicho utasaidia kuwapa uhakika wa bidhaa wanazoagiza na kupunguza kiwango cha fedha wanachopoteza kwa kuletewa mizigo yenye ubora hafifu.
“Unajua unapoagiza mzigo ukiwasiliana na msambazaji aliye China unakuwa hauna uhakika wa kupata asilimia 100 ya ubora ulioagiza, tofauti na sasa kukiwa na kituo na msambazaji akiwa hapa unaweza kudai fidia kama ulicholetewa hakikidhi ubora unaouhitaji,” amesema Ndimbo.