Rais Samia alivunja Bunge rasmi

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kulivunja rasmi Bunge Agosti 3, mwaka huu, kutoa nafasi ya uteuzi wa wagombea wa nafasi hiyo.

Taarifa ya kuvunjwa kwa Bunge inatolewa katika kipindi ambacho, vyama mbalimbali vya siasa nchini, vipo kwenye hatua za michakato ya ndani ya kuwapata wagombea wa ubunge, urais na udiwani.

Hata hivyo, hati hiyo ya kulivunja bunge imetolewa wakati ambao, zaidi ya wabunge 30 wameenguliwa katika mchakato wa ndani wa Chama cha Mapinduzi (CCM), huku wengine wakisubiri kura za maoni kujua hatima yao.

Hati ya kuvunjwa kwa Bunge hilo imetolewa leo, Jumatano Julai 30, 2025, ikiwa ni utekelezaji wa Ibara ya 92(2)a ya Katiba ya Tanzania inayompa Rais mamlaka ya kulivunja.

Katika hati hiyo, Rais Samia ameandika: “Kwa mujibu wa kifungu cha 49 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Sheria Na. 1 ya Mwaka 2024, uteuzi wa wagombea kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu hauwezi kufanyika isipokuwa kama Bunge limekwishavunjwa,” imeandikwa hati hiyo.

Kwa mujibu wa hatua hiyo, Ibara ya 90(2)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka, 1977, Rais anaweza kulivunja Bunge iwapo limemaliza muda wa uhai wake wa miaka mitano kwa mujibu wa Ibara ya 65 ya Katiba au wakati wowote ndani ya kipindi cha miezi 12 ya mwisho ya uhai wa Bunge.

“Hivyo basi, mimi, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mamlaka niliyopewa chini ya Ibara ya 90(2)(a) ya Katiba ninalivunja Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia tarehe 3 Agosti, 2025 ili kutoa fursa kufanyika kwa uteuzi wa wagombea katika Uchaguzi Mkuu na kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu,” imeandikwa hati hiyo.

Hatua ya kuvunjwa kwa Bunge hilo, inaashiria ukomo rasmi wa wadhifa wa ubunge kwa wabunge waliohudumu kuanzia mwaka 2020 hadi 2025 na kutoa nafasi ya kupatikana wengine.