Russia yaongeza ufadhili wa masomo kwa Watanzania

Dar es Salaam. Urusi imesema inaendelea kuongeza ushirikiano katika sekta ya biashara na elimu ili kuchochea fursa za kiuchumi na kielimu kwa Watanzania katika mkakati wake wa kuimarisha urafiki na ushirikiano wa kidiplomasia na Tanzania.

Hayo yamesemwa na Balozi wa Russia nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, leo Jumatano Julai 30, 2025, alipozungumza katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha urani kinachojengwa na Kampuni Mantra Tanzania Limited kutoka Russia, wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.

Amesema katika kuenzi urafiki wa muda mrefu baina ya Tanzania na Russia, nchi hiyo itaendelea kuongeza fursa za kielimu na kiuchumi kwa Watanzania.

“Katika kuendeleza ushirikiano baina ya nchi zetu mbili, imekusudia kuchochea fursa za kiuchumi na kielimu kwa manufaa ya watu wa mataifa yetu,” amesema.

Balozi Andrey amesema kupitia miradi ya kimkakati inayosimamiwa na nchi hiyo nchini ukiwemo wa urani uliozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan wilayani Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma utazalisha zaidi ya ajira 4,000 kwa Watanzania na kuongeza uzalishaji wa umeme, nchi hiyo inafungua ukurasa mpya wa ushirikiano wake na Tanzania.

Akizungumzia fursa za elimu, Balozi Andrey amesema Russia imeongeza fursa za ufadhili wa masomo kwa Watanzania kwenda kusoma fani mbalimbali katika taifa hilo kutoka nafasi 90 hadi nafasi 150 kwa mwaka huu wa elimu.

“Leo natangaza katika kuongeza ushirikiano wa muda mrefu baina ya mataifa haya mawili, Russia imeongeza nafasi za ufadhili wa masomo kwa vijana wa Tanzania katika mwaka wa masomo 2025/2026 kutoka nafasi za awali 90 hadi 150,” amesema balozi huyo.

Balozi Andrey amemshukuru Rais Samia kwa uongozi wake ambao ameutaja  kuendeleza ushirikiano mwema uliodumu kwa miongo kadhaa baina ya mataifa hayo, akiahidi nchi hiyo itaendelea kubuni fursa mbalimbali katika kudumisha ushirikiano huo.

Rais Samia akionesha kufurahishwa kwake na hatua hiyo, ametuma salamu za shukurani kwa Serikali ya Russia akisisitiza kuendeleza ushirikiano huo mwema ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.