ZIKIWA zimesalia siku tatu kabla ya kuanza kwa michuano ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN 2024), mjadala umeibuka kuhusu maandalizi ya Tanzania kama mwenyeji wa mashindano hayo kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.
Mjadala uliofanyika leo Julai 30, 2025 kwenye Mwananchi X Space wenye mada isemayo; ‘Maandalizi ya michuano ya CHAN 2024 yanaridhisha?’, wadau mbalimbali wa michezo, habari, uchumi, na hata wachezaji wa zamani wametoa maoni yao, wakielezea mapungufu, mafanikio, na fursa zilizopo wakati taifa likielekea katika tukio hili kubwa.
Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala amesema kwa kiasi kikubwa maandalizi yanaridhisha.
“Mkuu wa Mkoa wa Tabora ameungana na mashabiki kusapoti jambo hili muhimu ila kumekuwa na uelewa hata mitaani watu wanazungumzia sana hii michuano kwa sababu inafungua fursa kwa Wajasiriamali na Wafanyabiashara.
“Kwa hiyo tumefanikiwa, kwangu natoa asilimia 90, hizo zilizobaki ni za siku mbili zilizosalia, kila kitu naona kinaenda vyema ndio maana Wananchi wamewezeshwa kutoka mikoani kwenda Dar kuangalia mechi muhimu ya ufunguzi.
“Unaona watu wanavyoendelea kujiandikisha ili kusafiri kunatoa picha halisi namna ambavyo mashabiki wamevalia njuga suala hili, mwanzoni Stars ilikuwa inacheza lakini watu walikuwa hawapo uwanjani, ila sasa ni tofauti, naamini kabisa uwanja wa Benjamin Mkapa utakwenda kujaa,” amesema Mwagala.
Tanzania ambayo ni mwenyeji wa fainali hizo zitakazoanza Agosti 2 hadi 30 mwaka huu kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, itacheza mechi ya ufunguzi Agosti 2 dhidi ya Burkina Faso ukiwa ni mchezo wa Kundi B utakaoanza saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mwandishi Mwandamizi wa Habari za Michezo wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Charles Abel amesema kwa namna maandalizi yaliyofanyika hadi sasa anaona kabisa Watanzania wapo tayari kwa ajili ya Chan 2024.
Akiwa kama mchokoza mada wa mjadala huo, Abel amesema kwa mtazamo wake maandalizi yamekamilika kwa miundombinu kuanzia viwanja vitakavyotumika kwa michuano hiyo kama wenyeji yaani Benjamin Mkapa na New Amaan Complex, Zanzibar na hata viwanja vya mazoezi.
Amesema maboresho ya miundombinu ni ya kiwango cha hali ya juu na hata suala la ulinzi na usalama kupitia Polisi Kamanda wa Maalumu ya Dar es Salaam na hata kule Zanzibar wamehakikisha kila kitu kiko sawa.
Hata kwa upande wa mapokezi ya timu zilizowasili, nako kumekaa sawa kwani hakuna changamoto zozote zilizojitokeza na mwitikio ni mkubwa kwa sasa na mashabiki wana hamu kubwa.
Hata hivyo, amesema mwanzoni mwamko ulionekana kuwa mdogo, lakini kadri siku zinavyosonga mbele ndivyo mzuka umekuwa ukiongezeka, wakiwamo wakuu wa mikoa kuanzia Mwanza, Tabora na hata Dar es Salaam wamekuwa wakihamasisha na kununua tiketi mbali na kutoa mabasi ya kusafirisha mashabiki kwa fainali hizo jijini Dar es Salaam.
“Kwa haya yanayofanyika ni kuonyesha tupo tayari kwa fainali hizo na serikali inastahili pongezi kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika na hata kwa upande wa timu tumeonyesha tupo tayari kwa jinsi kambi ilivyofanyika Misri kisha iliporejea imecheza michezo ya Nchi Tatu iliyofanyika Zanzibar,” amesema Abel.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Hussein Ahmada Vuai amesema maandalizi kwa ujumla kwa ajili ya fainali za CHAN 2024 yapo vizuri na kwa Zanzibar mambo ni matamu zaidi kutokana na kupata uzoefu wa mechi za Kombe la Shirikisho Afrika walizoziandaa hivi karibuni.
Zanzibar ilianza mechi za nusu fainali kati ya Simba dhidi ya Stellenborch ya Afrika Kusini na baadae fainali iliyoikutanisha pia Simba na waliotwaa taji, RS Berkane ya Morocco, ndio maana kwa ZFF imekuwa ni rahisi kufanikisha maandalizi ya michuano hiyo ya CHAN 2024.
“Tumejiandaa vizuri hasa kuitangaza Zanzibar kwa sababu kwetu ni faida hasa kwa upande wa utalii, kila michuano mikubwa iliyokuja kucheza hapa kwetu, kuanzia ile ya Kombe la Shirikisho Afrika na tumekuwa na hamasa za ndani na nje ya uwanja,” amesema Vuai na kuongeza;
“Tumeandaa vikundi vya ngoma vinavyopokea timu uwanja wa ndege,lakini hata wakati wa mechi ili kuhakikisha kwamba wageni wanaona asili yetu.
“Kwa upande wa soka tumesitisha kila michezo ili kupisha mashindano hayo muhimu na kwa upande wa Televisheni za huku jambo litakalotangazwa ni mechi hizo.”
Katibu huyo amesema; “Maeneo ya biashara yameguswa kwa upande mkubwa,huwezi kuamini visiwani zimeshika kasi kuanzia chakula na nyingine,mfamo kama leo mmoja wa mfanyabiashara mkubwa wa hapa Zanzibar ameipa kambi ya Nigeria na wachezaji wote wamenunua viatu pia.”
Mdau wa masuala ya soka nchini, Carlos ‘Mastermind’ Sylvester, amesema ameridhishwa na maandalizi ya ujumla kwa ajilin ya mechi za CHAN 2024 kutokana na kila mdau kufahamu kuna michuano ya mashindano hayo Tanzania ikiwa nchi mwenyeji.
“Kuna mwingine alitamani kuona mabango yamewekwa kila sehemu ndio angeridhishwa, aone radio zote zizungumzie CHAN na wengine wanatamani kuambiwa waingie bure viwanjani ndio afurahie,” amesema Carlos na kuongeza;
“CHAN inaandaliwa na nchi tatu tofauti kama Tanzania ndio ingekuwa inasimamiwa yenyewe basi kelele zingesikika kila sehemu, lakini sisi ni ufunguzi wa mechi na nchi nyingine pia zina mechi nafikiri kwa upande wangu mambo yameenda vizuri na kilichobaki ni kuliamsha tu.”
Tanzania imepangwa kuanza fainali hizo kwa mechi ya ufunguzi wa fainali hizo dhidi ya Burkina Faso itakayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Fainali za nane za michuano ya Chan 2024 imepangwa kufanyika Jumamosi ya Agosti 2 katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda ikishirikisha timu za taifa za nchi 19 wakiwamo watetezi wa taji, Senegal na itafikia tamatui Agosti 30.
Katibu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Angetile Oseah amesema kuwa: “Naona kama watu akili yao kubwa iko kwenye timu ya Taifa kushiriki na tunakosea kwa sababu sio kitu tunachokitaka ila tulihitaji kuwa waandaji.
“Vigezo vya kupata haki ya kuandaa michuano ya CHAN huwa yanahatua zake na ni lazima upate msukumo kwa Serikali kwa sababu inahusu mambo mengi nje na uwanja.
“Wakati Brazil na Sauzi wanaomba kuandaa ilibidi washughulikie maswala ya kihalifu na Serikali yetu ilijitahidi sana kuzungumzia miundo mbinu na kuwahakikishia watu kwamba kila kitu kitakuwa sawa.
“Chama cha Soka Afrika kimekwama kwenye hamasa kuonyesha kwamba nchi kuna ujio mkubwa unakuja,ili wajiandae na tukio kubwa la ufunguzi na ukiangalia hatujafanya kitu zaidi ya kuhamasisha watu wa Mbagala.
“Hatujui nani amebuni maswala ya Utamaduni,watu wa ngapi wamefanya maswala ya VISA, hapa tunatakiwa tupime tumefikia wapi na kwangu ukiniuliza nitasema hatujafanikiwa kwenye maandalizi na kama watu wa mpira wamekaa kimya na Serikali ndio inaongea bado tunakazi ya kufanya.”
MAMBO MATATU YAMEANGUSHA MAANDALIZI
OFISA Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ ametaja mambo matatu yaliyoiangusha Tanzania ambayo ndio nchi mwenyeji wa michuano ya CHAN yanayotarajia kuanza Agosti 2 mwaka huu, ikiwamo suala la kutokamilika kwa ujenzi wa miundo mbinu ya barabara.
“Maandalizi kwa ujumla hayajaniridhisha ukizingatia sisi ndio nchi wenyeji kwa kuanzia miundo mbinu ambayo sio viwanja pekee inahusisha barabara ambazo kwa jiji la Dar es salaam ni changamoto kutokana na foleni,” amesema Zakazi na kuongeza;
“Ukiondoa hilo pia mashindano yamekosa hamasa tofauti na matarajio ya wengi ikiwa ni mara yetu ya kwanza kuandaa tukio kubwa kama hili, mji wa mashindano barabara zinakuwa zimekamilika lakini kwetu kuna ujenzi unaendelea foleni nimekuwa nyingi.”
Msemaji huyo wa Azam ameongeza kwa kusema; “Upande wa kuyafanya mashindano haya kuwa makubwa pia hatujawa tayari mfano leo tulikuwa tunampokea mchezaji wetu mpya, sio suala muhimu sana kuzungumza natoka nje ya mada, lakini mchezaji huyo amehoji mbona haoni shamra shamra kama Tanzania ni nchi mwenyeji, hakuna mabango ya kuvutia na kutambua kama kuna mashindano yanaandaliwa.
“Mabango hakuna mji umepoa kwa Tanzania hasa Dar es Salaam hakuna kinachoashiria mashindano wanasema nyumba yenye msiba utaijua tu lakini kwa ilivyo Tanzania hakuna kitu kama hicho.
Zakazi amesema hana wasiwasi na maandalizi ya kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars na kwamba anatarajia mambo mazuri kutokana na timu kujiandaa mapema, lakini nje ya uwanja hajavutiwa na kitu.
OFISA Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ ametaja mambo matatu yaliyoiangusha Tanzania ambayo ni miongoni mwa nchi mwenyeji wa michuano hiyo.
“Maandalizi kwa ujumla hayajaniridhisha ukizingatia sisi ndio nchi wenyeji kwa kuanzia miundo mbinu ambayo sio viwanja pekee inahusisha barabara ambazo kwa jiji la Dar es salaam ni changamoto kutokana na foleni,” amesema Zakazi na kuongeza;
“Ukiondoa hilo pia mashindano yamekosa hamasa tofauti na matarajio ya wengi ikiwa ni mara yetu ya kwanza kuandaa tukio kubwa kama hili, mji wa mashindano barabara zinakuwa zimekamilika lakini kwetu kuna ujenzi unaendelea foleni nimekuwa nyingi.”
Msemaji huyo wa Azam ameongeza kwa kusema: “Upande wa kuyafanya mashindano haya kuwa makubwa pia hatujawa tayari mfano leo tulikuwa tunampokea mchezaji wetu mpya, sio suala muhimu sana kuzungumza natoka nje ya mada, lakini mchezaji huyo amehoji mbona haoni shamra shamra kama Tanzania ni nchi mwenyeji, hakuna mabango ya kuvutia na kutambua kama kuna mashindano yanaandaliwa.
“Mabango hakuna mji umepoa kwa Tanzania hasa Dar es Salaam hakuna kinachoashiria mashindano wanasema nyumba yenye msiba utaijua tu lakini kwa ilivyo Tanzania hakuna kitu kama hicho.”
Zakazi amesema hana wasiwasi na maandalizi ya kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars na kwamba anatarajia mambo mazuri kutokana na timu kujiandaa mapema, lakini nje ya uwanja hajavutiwa na kitu.
Mchambuzi wa masuala ya michezo, Edo Kumwembe amesema maandalizi kwa timu yanaridhisha kwa sabababu wachezaji sikuhizi hawahitaji muda kujiandaa na wengi wanafahamiana huku wasi wasi mkubwa ukiwa ni hamasa.
“Tanzania ni watu wenye majivuno sana CHAN wanaona ni michuano midogo kwasababu haina mastaa makubwa tofauti na AFCON ambapo kutakuwa na mastaa wengi naamini wengi watafuatilia mashindano hayo kwa kufuata majina ya wachezaji wakubwa,” amesema na kuongeza;
“CHAN inashirikisha wachezaji wa ndani ambao wengi tayari wameshawazoea lakini kwa wachezaji wenyewe ni faida kwa wachezaji wenyewe kutokana na klabu walizotoka.
“Sina shaka kabisa na timu, kuhusu miundombinu nafikiri viwango vimefikiwa na ndio maana CAF wapo kimya.”
Naye Mhariri wa Habari za Uchumi na Biashara wa gazeti la Mwananchi, Ephrahim Bahemu ameyataja maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania kuwa sehemu ya kukwamisha maandalizi bora ya michuano ya CHAN 2025.
“Nafikiri mashindano haya yamekuja wakati mbaya kwani nchi iko katika harakati za uteuzi wa wagombea na inajiandaa na Uchaguzi Mkuu wa Taifa, hivyo ni ngumu kuwa na uzingativu ya pande zote mbili,” amesema Bahemu na kuongeza;
“Samahani sio kwa ubaya, lakini nakiri kuwa inawezekana hakukuwa na uzito katika uandaaji wa mashindano hayo kutokana na namna ambavyo mambo yanakwenda, kwani watu walikuwa bize na uteuzi na kusahau tukio hili muhimu.”
Bahemu amesema hakuna shamra shamra kuonyesha kama Tanzania ndio nchi mwenyeji kutokana na hamasa ndogo iliyopo, lakini bado kuna nafasi siku chache zilizobaki kwa waandaaji kuyapa kipaumbele mashindano haya.
TUSILAUMU MEDIA HAMASA CHAN
Mchambuzi wa masuala ya michezo, Edo Kumwembe amesema maandalizi kwa timu yanaridhisha kwa sabababu wachezaji siku hizi hawahitaji muda mrefu kujiandaa. lakini wasiwasi wake ni hamasa kwa mashabiki.
“Tanzania ni watu wenye majivuno sana, CHAN wanaona ni michuano midogo kwasababu haina mastaa makubwa tofauti na AFCON ambapo kunakuwa na mastaa wengi wakubwa kutoka Ulaya na kwingineko, naamini wengi watafuatilia mashindano hayo kwa kufuata majina ya wachezaji wakubwa,” amesema;
“CHAN inashirikisha wachezaji wa ndani ambao wengi tayari wameshawazoea lakini kwa wachezaji wenyewe ni faida kwa wachezaji wenyewe kutokana na klabu walizotoka.”
“Sina shaka kabisa na timu, kuhusu miundombinu nafikiri viwango vimefikiwa na ndio maana CAF wapo kimya.”
Edo amesema hawezi kuvilaumu vyombo vya habari kwamba vimefeli kuihamasisha michuano hii ya CHAN akisema: “Sijui sisi mashabiki wa Tanzania tulifeli wapi. Tunapezipenda klabu zetu Simba, Yanga kisha ndio Taifa Stars. Ni tofauti na wenzetu Uganda kwa mfano. Habari ya (Khalid) Aucho amewasili kujiunga na kambi ya timu ya taifa (The Cranes) ni habari kubwa kwa wenzetu Uganda kuliko usajili wa klabu zao kama Kampala City Council. Sisi vyombo vya habari vingi vinafanya kazi kibiashara. Vinaangalia soko liko wapi. Nimefanya kazi katika magazeti kwa miaka mingi. Ni ngumu kuweka kichwa cha habari kinachosema ‘Taifa Stars iko kamili’ ukategemea kuwavutia wanunuzi, hii ni ngumu. Mashabiki wanaonekana kuvutiwa zaidi na habari za klabu zao.”
Wakati kukiwa na mtazamo tofauti wa maandalizi kuridhisha au kutoridhisha, wadau hao wametoa suluhisho juu ya kitakachofanyika siku zilizobaki.
Angetile amesema: “Uuzaji wa tiketi kwenye mashindano haya uko kwenye mitandao zaidi na ni lazima tuongeze nguvu kubwa ili wajue kwamba kuna mechi zaidi ya 10 za raundi ya awali.
“Ili waweze kupata tiketi za mechi husika sio tu kwenda Mbagala na Tandika kuweka hamasa ila watu waambiwe yapo mataifa mengine yanacheza hapa na nini ambacho wanaweza kupata nje ya uwanja na maisha kwa ujumla ndani ya Tanzania.”
Fainali hizo zinatarajiwa kuanza rasmi Agosti 2 hadi Agosti 30 zikishirikisha timu za nchi 19 wakiwamo wenyeji Tanzania, Kenya na Uganda.
Kwa Tanzania, Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Dar utatumiwa na timu zilizopangwa Kundi B ambazo ni Tanzania, Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Pia Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar, utachezewa mechi za Kundi D zinazohusisha timu za Congo Brazzaville, Nigeria, Senegal na Sudan.
Kwa upande wa makundi mengine, yapo hivi; Kundi A: Kenya, Morocco, Angola, DR Congo na Zambia mechi zikichezwa Kenya na Kundi C ni Uganda, Algeria, Guinea, Niger na Afrika Kusini zitakazochezwa nchini Uganda.