Dar es Salaam. Serikali imewataka wakuu wa taasisi za umma kujiepusha kuwa miungu watu na badala yake watengeneze mazingira rafiki ya kazi yatakayowawezesha kuongeza tija na ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hiyo ni kwa sababu usimamizi mzuri wa rasilimali watu ndiyo njia itakayowasaidia kuongeza ufanisi wa taasisi walizoaminiwa kuziongoza.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, wakati akifunga mafunzo elekezi ya siku nne kwa wakuu wa taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali 114, kundi la pili, jana Jumatano, Julai 30, 2025.
Ridhiwani amesema ikiwa wakuu hao wa taasisi wanataka kupata matokeo mazuri na tija, ni lazima watengeneze mazingira rafiki kwa watu walio chini yao na si kuogopwa.
“Ikiwa mnataka kupata matokeo mazuri, mnapaswa kuepuka kuwa miungu watu na badala yake tengenezeni mazingira mazuri ambayo yatawahamasisha watumishi kujituma, kuleta ubunifu na kuongeza tija katika kila ngazi ya utendaji,” amesema na kuongeza kuwa hiyo haimaanishi kuwa wawachekee watu wanaoleta uzembe kazini.
“Ninachomaanisha ni nyie kufanya kazi kwa msukumo, weledi na kuzingatia misingi ya utawala bora,” amesema.
Waziri huyo amesema ni vyema wakuu hao wahakikishe wanazingatia maadili ya utumishi wa umma na kuhakikisha kila mfanyakazi anahisi kuheshimiwa, kuwa na nafasi ya kutoa mawazo yatakayoboresha huduma na kuleta mabadiliko chanya.
“Hii ni njia ya kuhakikisha taasisi zinakuwa na tija kwa muda mrefu na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kiutendaji,” amesema Ridhiwani.

Akizungumzia mageuzi yanayoendelea kufanyika katika kuimarisha utendaji kazi na usimamizi wa taasisi za umma, amesema yameongeza uwezo wa Serikali kufaidika na uwekezaji wa Sh86.29 trilioni.
Hili linadhihirishwa na gawio la mwaka wa fedha 2024/25, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alikabidhiwa Sh1.028 trilioni kama mapato yasiyo ya kikodi kutoka kwa taasisi, mashirika ya umma, wakala za Serikali na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa chache.
“Kiasi hicho ni cha kihistoria. Lengo letu la msingi ni kuhakikisha kuwa uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma unaendelea kuleta tija kwa Taifa letu kwa mfumo endelevu,” amesema.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi), Juma Mkomi, amesema mafunzo yaliyotolewa kwa wakuu hao wa taasisi ni kitendea kazi muhimu kwani tangu walipoteuliwa hawakuwahi kupatiwa mafunzo rasmi.
“Mafunzo haya ni muhimu kwani yamegusa rasilimali watu na usimamizi wa taasisi. Mafunzo yataongeza ufanisi na usimamizi wa rasilimali watu kwa ajili ya kuleta tija kwa taasisi na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa miongozo ya Serikali na sheria zinazohusu usimamizi wa taasisi, kwa lengo la kudhibiti matumizi yasiyo na tija na kuimarisha usimamizi wa rasilimali za umma kwa manufaa ya Taifa.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema ili kufanikisha safari ya mageuzi ya mashirika ya umma, inahitajika uongozi thabiti, ubunifu, na mshikamano wa pamoja kati ya taasisi za umma, wizara mama, Ofisi ya Msajili wa Hazina na wadau wengine wa Serikali.
Amewahimiza watendaji wakuu kuendelea kujifunza na kubadilisha mtazamo wao ili kuendana na mageuzi ya utawala bora yanayohitajika kufanikisha maendeleo endelevu ya Taifa.
“Tunaweza kuupata ufanisi wa matokeo chanya kama uongozi utakuwa na ufanisi. Sisi kama Ofisi ya Msajili wa Hazina tutaendelea kufanya mageuzi ili taasisi zilete tija iliyokusudiwa,” amesema.
Alipofungua mafunzo hayo Julai 28, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, alisema Serikali imedhamiria kuanzisha mfumo wa upimaji kwa kutumia mitihani ya lazima kwa maofisa walioteuliwa au kupandishwa vyeo vya uongozi.
Hatua hiyo mpya ni sehemu ya kuhakikisha watu wenye uwezo na uelewa thabiti wa shughuli za utumishi wa umma ndiyo wanaokabidhiwa majukumu muhimu ya kuendesha taasisi au mashirika ya umma.
“Hivi ndivyo inavyofanyika duniani kote. Maendeleo katika nchi yoyote huanza na sekta ya umma yenye nguvu. Tuko mbioni kuanzisha mitihani kwa viongozi baada ya kuteuliwa au kupandishwa vyeo kwa lengo la kuboresha ufanisi na kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa,” alisema Dk Kusiluka.