MABOSI wa Fountain Gate wapo katika mazungumzo ya kumuajiri aliyekuwa kocha mkuu wa 1472 FC ya Nigeria, Ortega Deniran, ili kukiongoza kikosi hicho msimu ujao akichukua nafasi ya Mohamed Ismail ‘Laizer’ aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo kumalizia msimu uliopita.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, zimeliambia Mwanaspoti Ortega ambaye ni raia wa Nigeria amepewa mkataba wa mwaka mmoja wa kukiongoza kikosi hicho, ambapo muda wowote kuanzia sasa atatua Tanzania kwa ajili ya kuanza maandalizi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Fountain Gate, Wendo Makau alisema wapo makocha mbalimbali waliotuma maombi yao ya kupata kazi kikosini humo, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano yaliyofikiwa kwa sababu wanahitaji kufanya uamuzi sahihi.
“Msimu uliopita hatukufanya vizuri na presha ya kushuka daraja unaona jinsi ilivyokuwa kubwa, sasa hili hatuhitaji tena kuona linatokea, tunaendelea na vikao vyetu vya bodi ya wakurugenzi na tukikamilisha tutaweka wazi hilo,” alisema Wendo.
Licha ya kauli ya Wendo, Mwanaspoti linatambua katika mchujo wa makocha sita walioomba, Ortega ndiye aliyepitishwa ili kuiongoza timu hiyo, ingawa sharti alilopewa ni kuja na kocha mmoja wa makipa au wa viungo tu na wala sio msaidizi.
“Ortega alitaka kuja na benchi lake lote la ufundi lakini uongozi ulimwambia achague mmoja tu kati ya kocha wa makipa au wa viungo ili kupunguza gharama, suala la msaidizi wake atabaki Laizer kutokana na heshima yake,” kilisema chanzo chetu.
Ortega alizaliwa Mei 28, 1986, huko Warri, Nigeria, ambako alikuwa anacheza nafasi ya ushambuliaji, akizichezea timu za Alacranes Rojos de Apatzingan, Lagartos de Tabasco zote za (Mexico), CD Suchitepequez (Guatemala) na Chongqing Lifan ya China.
Timu nyingine ni Spartak Varna, Slavia Sofia, PFC Levski Sofia zote za Bulgaria, FC Urartu ya Armenian, Dolphin FC ya kwao Nigeria na Edinburgh City FC ya Scotland, huku akifundisha Warri Wolves, Sporting Lagos na 1472 FC zote za Nigeria.
Ortega alianza taaluma ya ukocha akiwa benchi la ufundi la Edinburgh City na kushinda ubingwa wa Lowland League msimu wa 2014–2015 na 2015–2016 na kupanda Ligi Kuu ya Scotland, huku mwaka uliofuata wa 2017 akajiunga na Enyimba FC ya Nigeria.