BAADA ya kutua Pamba kuchukua mikoba ya Fred Felix ‘Minziro’, Mkenya Francis Baraza ameutaka uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha wanambakiza kipa namba moja wa timu hiyo, Yona Amos.
Baraza aliyeingia makubaliano ya mwaka mmoja kuinoa Pamba, alitambulishwa rasmi juzi Julai 30, 2025, katika ofisi za halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Baraza aliyewahi kuzinoa Dodoma Jiji, Biashara United, Kagera Sugar na Tanzania Prisons, katika kibarua chake Pamba atasaidiana na Temi Felix (kocha msaidizi), John Waw (kocha wa makipa), Shaban Kado (kocha wa makipa msaidizi) na George Aaron (kocha wa viungo).
Kipa, Yona Amosi alikuwa mmoja ya wachezaji wa Pamba Jiji chini ya Minziro, akiongoza kwa kuhusika katika mechi nyingi (28) za timu hiyo.
Akizungumzia mipango yake klabuni hapo, Baraza alisema tayari amefanya mazungumzo na uongozi wa timu hiyo na kuwaeleza nia yake ya kumhitaji kipa huyo, hivyo, anatakiwa kubaki kwa namna yeyote ile.
“Tangu jana (Jumanne) nimewaambia sitaki Yona (Amosi) aondoke maana ni kipa mzuri, uwepo wake kwa kiwango alichonacho ni bora na atatusaidia. Pia tumepata kocha mzuri wa makipa (John Waw) namfahamu akiwa Kagera Sugar kwa hiyo itakuwa ni faida kwa timu,” alisema Baraza.
Kocha huyo alisema tayari ameshakabidhiwa majina ya wachezaji wote wa timu hiyo, kuyapitia na kutoa mapendekezo kwa uongozi maeneo ya kuboresha na kuongeza majina kwenye dirisha la usajili.
“Meneja ameshanipa majina ya wachezaji tunajua wapi pa kuanzia, Pamba nimeifuatilia ni timu nzuri lazima tushikane sisi wana Mwanza,” alisema Baraza na kuongeza;
“Tukiweza kufanya kazi yetu vizuri kwa kushirikiana matokeo yatapatikana na Pamba ina uwezo wa kumaliza katika nafasi tano bora, hilo naliona.”
Mwenyekiti wa Pamba, Bhiku Kotecha alimtoa hofu kocha huyo kwa kumhakikishia uongozi utampa ushirikiano wa kutosha na hautamuingilia wala kumpangia cha kufanya kwenye kikosi chake.
“Tumemwambia walimu sisi uongozi hatutamuingilia katika mipango yake ya timu tunachotaka ni atufanyie kazi tupate matokeo.