Wanaoguswa msamaha wa adhabu, riba watakiwa kuzingatia muda

Unguja.  Baada ya Serikali kufuta riba na adhabu kwa walipakodi wenye malimbikizo ya madeni ya kodi, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), imewahimiza wahusika kutumia fursa hiyo kuyalipa ndani ya muda uliotolewa.

Kwa mujibu wa tamko la Serikali namba 84 la mwaka 2025, imefuta riba na adhabu kwa walipakodi wote wenye malimbikizo ya madeni ya kodi katika mamlaka hiyo, msamaha utakaodumu kwa miezi sita kuanzia Julai Mosi, 2025 hadi Desemba 31, mwaka huu.

Wakati akiwasilisha bajeti ya Serikali katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Juni 12, 2025, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya alisema uamuzi wa Serikali unalenga kuwapa fursa wafanyabiashara waliolimbikiza madeni kupata mwanya wa kuyalipa.

Kwa mujibu wa Dk Saada, hatua hiyo pamoja na kuwapa fursa wafanyabiashara kuendesha biashara zao kwa amani, lakini itaongeza mapato ya Serikali.

Katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Julai 31, 2025 na ZRA imewahimiza wafanyabiashara kutumia muda uliopangwa kabla ya kumalizika kwani itawasaidia kuanza upya na kupanga mienendo ya biashara zao kwa utulivu bila usumbufu.

Taarifa hiyo iliyothibitishwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Walipakodi ZRA, Makame Khamis Moh’d, imesema msamaha wa adhabu na riba utatolewa kwa asilimia 100, hivyo mlipakodi atahitaji kulipa kiwango cha kodi ikiwa ni deni halisi baada ya kutolewa riba na adhabu.

“Watu hawa watahudumiwa na kamati maalumu iliyoteuliwa kufanya kazi hii, kutakuwa na fomu maalumu za kuomba punguzo hilo, kama ilivyo kawaida ofisi za ZRA zinakuwa wazi siku zote kwa Unguja inatumika ofisi kuu Mazizini na Pemba inatumika ofisi kuu Gombani,” amesema.

Hata hivyo, ZRA imesema msamaha huo utahusu walipakodi waliotimiza masharti na taratibu ambazo zitajadiliwa na kukubalika kati ya Kamishana Mkuu na mlipakodi.

Baadhi ya wafanyabiashara wamesema ni fursa nzuri ambayo wanatakiwa kuichangamkia kwani itawasaidia kusawazisha madeni yao na kuanza upya.

Mmoja wa wafanyabiashara eneo la Malindi, Fat-hiya Khamis Ali amesema jambo hilo si la kufanyia mchezo, kwani litawasidia katika mtiririko wa biashara.

“Malimbikizo yakiwa makubwa inaondosha hata ari ya kufanya biashara lakini hii ni fursa nzuri mtu anatakiwa ajisafishe ili kuendelea kufanya biashara kwa kujiamini na uaminifu,” amesema.