Arusha. Askari wa wanyamapori nchini wametakiwa kuongeza uzalendo na uadilifu katika kulinda rasilimali hizo muhimu kwa mustakabali wa taifa ili ziendelee kuongeza mapato ya Taifa yatokanayo ya utalii.
Aidha, wadau wa utalii ikiwemo taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wametakiwa kuhakikisha wanachukua hatua za kiuhifadhi hasa katika mazingira haya ya mabadiliko ya tabianchi, migogoro ya binadamu na wanyamapori pamoja na vitisho vya kiusalama.
Maagizo hayo yametolewa jana Alhamisi Julai 31, 2025 na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Dk Robert Fumagwa katika maadhimisho ya kimataifa ya Siku ya Askari wa Wanyamapori duniani, yaliyofanyika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Amesema siku hiyo huadhimishwa kila mwaka kama kumbukizi kuwaenzi askari waliopoteza maisha na wengine kujeruhiwa wakitekeleza majukumu yao.
“Tunawapongeza askari wanaendelea kuzipambania rasilimali hizi usiku na mchana kuhakikisha zinaendelea kuwepo kwa mustakabali wa taifa letu, uzalendo na uadilifu ndiyo nguzo ya kuhifadhi hazina hii, niombe kila mmoja atimize wajibu wake,” amesema.

Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Dk Robert Fumagwa akizungumza katika maadhimisho ya Kimataifa ya Askari wa Wanyamapori Duniani, yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
“Leo tunawakumbuka mashujaa waliolala mbele za haki, tunaendelea kutambua mchango wa askari waliopo kazini na tunawapa moyo askari wote kuendelea kuwa majasiri, wenye welezi na wazalendo katika kulinda urithi wa asili wa taifa letu, wadau tuunganishe nguvu,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya uhifadhi, kuanzishwa kwa vituo vya kisasa vya ufuatiliaji doria, kuimarishwa kwa ushirikiano na vyombo vya ulinzi na usalama katika operesheni za kupambana na ujangili.
“Pamoja na mafanikio yaliyopatikana bado sekta ya uhifadhi inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo migogoro kati ya binadamu na wanyamapori, vitisho kutoka kwa majangili, mifugo kuingizwa hifadhini kwa ajili ya malisho na mabadililo ya tabianchi yanayoathiri mfumo wa ikolojia,” amesema mjumbe huyo.
Mjumbe huyo amesema kazi za uhifadhi nyingi ni mtambuka zinahitaji kila mmoja kushiriki kukabiliana nazo kwani kusipokuwa na uhifadhi thabiti Tanzania haitapata watalii na Serikali itakosa mapato yatokanayo na utalii.
Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi Tanapa, Musa Kuji amesema kwa mwaka 2024/25 Tanapa ilivuka lengo na kukusanya Sh500 bilioni ambapo makadirio yao yalikuwa Sh430 bilioni na kuwa wanatarajia kuendelea kukuza mapato kutokana na sekta hiyo kukua.
Amesema Serikali imekuwa ikiboresha maslahi yao na kuwa wao kama watumishi wana wajibu wa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa bidii, weledi, uaminifu na uadilifu.
“Kiukweli tuna Jeshi Usu linafanya kazi na la mfano wa kuigwa, linafanya kazi ya kuhifadhi maliasili zilizopo pamoja na usalama wa taifa letu. Hifadhi nyingi ziko mipakani, hivyo tunapoadhimisha siku ya leo tukumbuke vijana wetu wanalinda na amani ya nchi.
Mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Fidel Kimario amesema Tanzania inajivunia matunda na ujasiri wa utendaji kazi wa Askari wa Wanyamapori na Serikali itaendelea kusimama nao kulinda rasilimali.
“Tanzania tunajivunia matunda ya ujasiri wao na tunachokiona kwenye sekta ya uhifadhi siyo kitu chepesi, Tanzania tuna nafasi ya kujivunia rasilimali tulizonazo lakini lazima tutambue mchango wao mkubwa kwenye uhifadhi. Niwatie moyo askari wa wanyamapori pamoja na changamoto mnazokutana nazo Serikali inasimama na nyie kulinda na kuhifadhi rasilimali,” amesema.
Katika maadhimisho hayo, askari wa wanyamapori 40 waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali walipewa vyeti na fedha taslimu Sh1 milioni kila mmoja, wakiwemo askari hodari walioanzisha na kuongoza vikosi maalumu vya doria, kudhibiti na kukomesha ujangili ndani ya hifadhi.
Wengine ni waliofanya matukio ya kishujaa ikiwemo kuokoa maisha ya askari wenzao, wageni pamoja na kuokoa mali za wageni, shirika katika mazingira hatari ambapo pia Tanapa walitoa cheti na zawadi hiyo kwa askari wa kwanza wa kike Tanapa, Asha Mnkeni aliyeanza mwaka 2005.