Serikali yacharuka ukatili wa kijinsia, maelfu wakiokolewa

Mbeya. Wakati watu 3,735 wakiokolewa na vifo vya mama na mtoto kupitia mpango wa Dharura Fasta, Serikali imetaka wanaofanya ukatili wa kijinsia kuripotiwa na kuchukuliwa hatua za kisheria haraka.

Pia, imesema ili kuondokana na wimbi kubwa la watoto mitaani, wazazi na walezi waelimishwe juu ya upendo na ushirikiano kwenye ndoa badala ya kuishi kwa migogoro.

Akizungumza jana Julai 31, 2025 katika hafla ya uzinduzi wa nyumba ya shirika la Himso jijini Mbeya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Benno Malisa, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema kwa sasa idadi ya watoto mitaani inazidi kuongezeka.  

Amesema sababu kubwa ni kutokana na kutokuwa na upendo kwenye ndoa, huku akibainisha kuwa kumekuwapo na vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo wanaofanya hivyo huingia makubaliano na wazazi kuficha unyama huo.

“Elimisheni wanandoa kuishi kwa upendo ili kuondokana na wimbi la watoto mitaani, lakini ripotini haraka wanaofanya ukatili kwa watoto kisha kubagaini na wazazi ili vyombo vya dola na serikali ichukue hatua za kisheria,” amesema Itunda.

Hata hivyo, mkuu huyo hakusita kuipongeza shirika la Himso kwa uwajibikaji akieleza kuwa kupata ofisi yake rasmi itaweza kuongeza ufanisi katika majumuku na kwamba Serikali itaendelea kuiunga mkono.

“Mabadiliko haya yanaonyesha uimara wa uongozi wa Himso, endeleeni kuhamasisha wananchi katika kujiunga na mifuko ya afya, kazi yenu ni kama ibada, nimesikia ajira zaidi ya 20 mmetoa, serikali itaendelea kuwaunga mkono,” amesema Itunda.

Mwenyekiti wa Bodi ya Himso, Dk Yahya Ipuge amesema tangu 2017 hadi Juni 2025, watu 3,735  wameokolewa na vifo kwa kupewa huduma hiyo kupitia mpango wa Dharula Fasta ikiwamo wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kwa wilaya za mikoa ya Mbeya na Songwe.

Amesema mpango huo ambao unalenga kupunguza vifo hasa kwa wagonjwa waishio vijijini, wamesajili wananchama 63,234 waliojiunga na mpango huo, huku vijiji 683 vikijisajili.

“Mpango wa dharura fasta ni huduma inayotolewa kwa mgonjwa kutoka nyumbani hadi hospitali, Serikali ndio watekelezaji sisi ni wasaidizi tu, tangu shirika letu kuanza 2012, tuliweka mradi huu kunusuru wananchi, ambapo tangu 2017 hadi Juni 2025, tumefikisha huduma kwa watu 3,735 katika wilaya 10 za mikoa ya Mbeya na Songwe.

“Kutokana na mafanikio haya, uongozi umepambana kupata wadau waliotuwezesha kupata jengo letu ambalo ni ofisi rasmi iliyogharimu zaidi ya Sh75 milioni ikiwa na uwanja maalumu wa kujenga kituo cha mafunzo, hivyo tunaomba Serikali iendelee kutuunga mkono,” amesema Dk Ipuge.

Dk Ipuge amesema pamoja na takwimu hiyo, lakini bado idadi si kubwa sana ambapo wanaendelea kuiomba jamii kujiunga katika bima ya afya kwa wote.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, John Mwaijulu amesema shirika hilo limekuwa na mchango mkubwa katika utoaji huduma kwa wilaya tano za mkoani humo akieleza kuwa hali hiyo imesaidia Serikali katika juhudi za kufikisha huduma za afya kwa wananchi.

“Tunaipongeza shirika hili limekuwa na mchango mkubwa kwa wilaya zetu tano za mkoa wetu wa Songwe, hali hii imeisaidia Serikali kufikisha huduma za afya kwa wananchi,” amesema Mwaijulu.

Naye Mkurugenzi wa Mtandao na Malezi, Makuzi na Maendeleo kwa Watoto (TECDEN), Maajuma Kibwana amesema kama Taifa bado wanahitaji mkubwa wa wadau ikiwamo Himso kutoa mchango kwa Serikali akikiri uwapo wa changamoto katika ufadhili kwa mashirika.

“Tunaamini wadau ikiwamo Himso na wengine wanaweza kukaa na kuchakata mawazo yenye kulipeleka mbele Taifa, tuendelee kutoa huduma kwa watoto na jamii kwa ujumla,” amesema Mwajuma.