Samia awatoa hofu wafanyabiashara Kariakoo ujio wa EACLC

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo hakijaanzishwa kushindana na Soko la Kariakoo, bali kuimarisha biashara na kuwa mfano wa kufundisha namna bora ya kuendesha masoko makubwa nchini.

“Kuwepo kwa kitu hiki si mshindani wa Soko la Kariakoo. Soko la Kariakoo limejenga jina kwa muda mrefu, lakini bado linahitaji kujifunza kutokana na uwepo wa kituo hiki. Kwa hiyo kituo hiki, badala ya kuwa mshindani wa Kariakoo, kiwe mwalimu wa soko la Kariakoo. Kwenye kituo hiki hatutegemei mapato ya Serikali kuvuja,” amesema Samia.

Rais Samia amesema kauli hiyo leo Ijumaa, Agosti 1, 2025, wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kikubwa cha biashara kinachotarajiwa kuongeza ajira na mapato ya Taifa.

Pia, amewataka wazalishaji nchini kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakuwa na ubora unaoendana na hadhi ya jina la Tanzania.

“Zalisheni kwa viwango, nisisitize kuzalisha kwa viwango sababu bidhaa yoyote itakayotoka na alama au maneno kwamba imezaliwa Tanzania lazima itoke na viwango kama jina letu lilivyo na viwango,” amesema.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza), Gilead Teri, amesema uwekezaji katika Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam umeingiza mtaji wa Sh282 bilioni na kutoa ajira zaidi ya 2,000 wakati wa ujenzi.

“Kukamilika kwa kituo hiki tunatarajia ajira za moja kwa moja 15,000 na zisizo za moja kwa moja 50,000, vizimba 2,060, ambapo zaidi ya 400 bilioni fedha za kigeni zitapatikana kila mwaka pamoja na zaidi ya 25 bilioni mapato ya Serikali (bila kujumuisha VAT),” amesema Teri.