Dar es Salaam. Wakati Sekretarieti ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, imeelekeza kurudishwa kwa watiania wote wa udiwani waliokuwa wameenguliwa wakapigiwe kura za maoni, wadau wa siasa wanasema uamuzi huo ni kiashiria kwamba kulikuwa na hila wakati wa uteuzi.
Uamuzi wa sekretarieti umefungua milango kwa makada wote waliochukua fomu kuomba nafasi ya udiwani katika kata 3,990 nchini kuomba kura kwa wajumbe, ili wapigiwe kura za maoni, kisha kusubiri uamuzi wa mwisho wa chama hicho.
Hatua hiyo imefikiwa Agosti mosi, 2025 baada ya Julai 29, 2025 baadhi ya majina ya wagombea nafasi ya udiwani ndani ya CCM kuwekwa hadharani tayari kwa kura za maoni Agosti 4, hatua ambayo imezua malalamiko na maandamano katika baadhi ya kata.
Utaratibu wa uchaguzi ndani ya CCM ni kufanya mchujo wa majina ya wagombea ubunge, uwakilishi na udiwani ambao awali, katiba ilitaka majina matatu yarejeshwe kwa kura za maoni kabla ya kufanya marekebisho ambayo yameruhusu kuopitishwa majina zaidi, kama ambavyo vikao vya kamati kuu na halmashauri kuu vitaona inafaa.
Wakati mabadiliko hayo yanafanyika, kwa upande wa udiwani mchakato wa kupitisha majina matatu ulikuwa umekamuilika, hivyo ilimuliwa uendelee ulipokuwa umefikia na kuibua manung’uniko.
Tangu Jumatano Julai 30, 2025 baadhi ya maeneo yameripotiwa kuwapo maandamano na mabango yenye ujumbe wa kutaka majina ya ‘watu wao’ yarejeshwe.
Miongoni mwa maeneo yalikoibuka malalamiko ni Kata ya Kunduchi mkoani Dar es Salaam ambako yalifanyika maandamano hadi zilipo ofisi za CCM za mkoa huo kulalamikia hatua ya Michael Urio kukatwa. Baadaye alirudishwa.
Julai 31, wakazi wa Kata ya Muze wilayani Sumbawanga Vijijini mkoani Rukwa, walizuia msafara wa viongozi wa CCM, wakilalamikia mchakato wa uteuzi wa majina ya wagombea udiwani katika kata hiyo.
Kilio chao kilitokana na kilichodaiwa kuwa orodha ya awali ya wagombea watatu iliyotangazwa Julai 29 ilibadilishwa asubuhi ya Julai 30 na jina la mgombea wa nne kuongezwa.
Jijini Dodoma, wakazi wa Kizota waliandamana kushinikiza jina la Jamal Ngalya aliyewahi kuwa naibu meya na diwani wa kata hiyo lirejeshwe.
Hayo yakijiri, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ya Agosti mosi, alitoa taarifa ikielekeza kurudishwa kwa watiania wote wa udiwani waliokuwa wameondolewa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uamuzi huo umetokana na kikao cha Sekretarieti ya taifa ya chama hicho iliyoketi Julai 31 kwa mtandao kupitia malalamiko ya wanachama.
Katika taarifa hiyo, Makalla amesema makatibu wa chama hicho mikoa, wanaelekezwa kuwarejesha watiania wote wa udiwani waliopitishwa na kamati za siasa za mikoa, ili wakapigiwe kura za maoni.
“Wagombea wote waliopo kwenye orodha ya awali waliyotumiwa makatibu wa mikoa wa CCM, warejeshwe ili wakapigiwe kura za maoni,” imeeleza taarifa hiyo.
“Aidha, kikao hicho kimefuta maelekezo yote yaliyotolewa awali. Hivyo, kinawaelekeza makatibu wa mikoa wa CCM wote nchi nzima kuzingatia na kutekeleza maelekezo ya sasa,” imeeleza taarifa.
Akizungumzia hatua hiyo, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Anjali Nguyuhambi amesema uamuzi wa sekretarieti unaonyesha kulikuwa na harufu ya hila zilizofanywa katika uteuzi wa watiania wa udiwani.
Amesema watiania waliokuwa chaguo la wananchi walikatwa na vikao viliamua kuwapitisha ‘watu wao’ na haijulikani kwa masilahi gani.
Kwa sababu hiyo, ameeleza wanachama waliibua malalamiko hadi zilipo ofisi za CCM, ndiyo uamuzi wa sekretarieti ikaelekeza makatibu wa mikoa warudishe watiania wote+1.
“Nilitarajia uamuzi huu ungefanywa pamoja na ule uliowahusisha wagombea kwenye nafasi za ubunge. Kwa kuwa umefanyika baada ya ule wa ubunge, pengine tafsiri yake ni kusikiliza maoni kutoka chini kama inavyoonekana kulikuwa na malalamiko ili kuondoa uwezekano wa watu kuondolewa kwa hila,” amesema.
Kutokana na uamuzi huo, Dk Nguyuhambi amesema itarajiwe kuona watiania waliopitishwa awali wakianguka na wale walioruhusiwa mwishoni wakipenya katika kura za maoni, kwani ndiyo wanaohitajika.
Uamuzi huo ni kama mbinu ya kujisahihisha, lakini wakati huohuo unaashiria kuwapo shida ndani ya uamuzi wa chama hicho, kama inavyoelezwa pia na mchambuzi wa masuala ya siasa na uongozi, Philemon Mtoi.
Mtoi anajenga mtazamo wa kujisahihisha, akisema wananchi wamelalamika na chama kimeona kisahihishe makosa kwa matakwa ya wengi.
Hata hivyo, amehoji ilikuwaje vikao vya chama hicho vifanye uamuzi usiowaridhisha wanachama wengi kiasi cha wengine kuandamana na baadhi kulalamika.
“Hivi ni viashiria visivyotoa taswira nzuri ndani ya chama husika. Kwa sababu inaonekana vikao vilipitisha watiania kwa utashi wake bila kuangalia kukubalika kwao, hili ni tatizo,” amesema.
Amesema chama hicho kwa kujisahihisha, kimeokoa mpasuko na kukosa kura za wananchi, ambazo pia ndizo zinazoamua ushindi hata wa nafasi ya Rais.
Kwa maneno mengine, amesema CCM iliamua kufanya mchujo bila kusikiliza wala kujali wananchi. Ukiwarudishia watu watiania watatu wawapigie kura, unawapunguzia machaguo.
“Nafikiri sekretarieti ya CCM imegundua kwamba kuna mchezo mchafu umechezwa katika madiwani, ndiyo maana imeamua kuchukua hatua za haraka,” amesema.
Wakati huohuo, watiania wa udiwani na ubunge wanaendelea kujinadi kwa wajumbe wakinadi sera zao.