Na Mwandishi wetu
WASANII wa muziki wa Singeli wanajiandaa kutikisa jukwaa la michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024 kwa tamasha kabambe litakalowatangaza kitaifa na kimataifa, ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa michuano hiyo mikubwa ya soka barani Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema kuwa wasanii wa Singeli watapata fursa ya kutumbuiza katika ufunguzi wa CHAN, huku Serikali ikiwa imechukua hatua rasmi kuwasilisha maandiko kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ili muziki huo wa asili ya Tanzania utambuliwe kama urithi wa taifa.
“Tunapenda kuona utamaduni wetu, hasa kupitia muziki wa Singeli, unapata heshima inayostahili. Kwa sasa tumepeleka maombi UNESCO ili utambulike kama urithi wa taifa, na tunafurahi kuona unapata nafasi ya kuwakilishwa kimataifa kupitia CHAN,” amesema Msigwa.
Mbali na maonesho ya muziki wakati wa ufunguzi wa michuano hiyo, Msigwa ametangaza kuwa kutakuwa na Singeli Festival, tamasha maalum litakalofanyika sambamba na michuano hiyo, likiwa na lengo la kuutangaza, kuuenzi na kuendeleza muziki wa Singeli, unaochukuliwa kama sauti ya mitaa ya Tanzania.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmon Mapana, amesema hatua ya kuwashirikisha wasanii wa Singeli katika CHAN ni mwanzo wa safari mpya kwa muziki huo, akibainisha kuwa Baraza hilo linatarajia kuandaa tuzo maalum za Singeli ili kuongeza hamasa na kuthamini vipaji vya wasanii wa muziki huo.
Kwa upande wake msanii wa Singeli, Manfongo, ameeleza walivyofurahishwa na fursa hiyo na kuahidi kutoa burudani kabambe kwa wageni na watanzania watakaofika siku hiyo.
“Niwaambie tu watanzania wenzangu wajitokeze kwa wingi siku ya ufunguzi wa CHAN na sisi tumejipanga vizuri kuwapa burudani ya kutosha kwenye tamasha la Singeli,”
Wasanii zaidi ya 15, wajarajiwa kutoa burudani siku hiyo, wakiwamo Dogo Paten, Miso Misondo, Wamoto Musiki, Mbosso, Shoro Mwamba na Meja Kunta.