Yajue magari yaliyopewa msamaha na TRA

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa msamaha wa kodi kwa magari yaliyoingizwa Tanzania bila kukidhi matakwa ya Sheria ya forodha ikiwamo yaliyoingizwa nchini kwa muda bila kurudishwa yalikotoka.

Mengine ni yale magari yaliyoingia Tanzania Bara kutokea Zanzibar bila kufuata taratibu za kiforodha, yaliyoingizwa nchini kwenda nchi nyingine (transit) na yakabakizwa au kutelekezwa Tanzania.

 Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Agosti Mosi, 2025 kwa umma na TRA, imeyataja magari mengine kuwa ni yale yaliyosamehewa kodi lakini umiliki wake umehamishiwa kwa watu wasiostahili kupewa msamaha na yaliyoingizwa nchini kwenda nchi nyingine ambayo muda wake umeisha na hayakupata kibali cha nyongeza.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda aliyesema msamaha huo wa kodi utakuwa kwa kipindi cha kuanzia Agosti Mosi, 2025 hadi Desemba, 2025.

Katika taarifa hiyo, Mwenda amefafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 70(1) cha Sheria ya Utawala wa Kodi Sura 438 na Kifungu cha 249 cha Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004, Kamishna Mkuu wa TRA anatoa msamaha wa kodi (Amnesty) kwa wamiliki wa magari ya aina yaliyoanishwa.

Bosi huyo wa TRA, amefafanua kuwa katika kipindi cha msamaha huo wamiliki wa magari husika watawajibika kulipa kiasi cha ushuru na kodi husika, bali kiasi cha riba na adhabu vyote vitasamehewa.

“Hivyo wamiliki wanatakiwa kufika katika ofisi za TRA zilizo karibu nao wakiwa na ushahidi wa umiliki pamoja na nyaraka za uingizwaji nchini wa magari husika, kwa ajili ya kukadiriwa ushuru na kodi stahiki,” amesema.

“Kwa magari yaliyo kwenye makundi tajwa yatakayokamatwa baada ya Disemba 31, 2025 ambayo ushuru na kodi zake hazikulipwa kikamilifu yatashughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Mbali na mashtaka ya jinai, watawajibika kulipa ushuru na kodi ikiwa ni pamoja na riba na adhabu,” ameeleza Mwenda.