Wakazi wa Mbezi, Kimara kupata ahueni ya foleni

Dar es Salaam. Wakati wakazi wa Mbezi na Kimara wakikumbana na adha ya foleni, Serikali imesema ujenzi wa njia nane katika Barabara Morogoro kutoka Ubungo – Kimara yenye urefu wa kilomita 5, umefikia asilimia 60.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa, Agosti Mosi, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akifungua Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo Dar es Salaam.

“Rais tulikuja kukulilia kuhusu foleni ya Mbezi na ulitoa maelekezo kwamba Tanroads watangaze kwa haraka sana, mkandarasi anayeweza kujenga kwa haraka barabara hii ya kilomita 5 kutoka Ubongo mpaka Kimara ili kuunganisha barabara nane,” amesema na kuongeza;

“Barabara hii sasa iko zaidi ya asilimia 60, mkandarasi amejenga chemba 280 zinazoachana kwa mita 35 na inatengenezwa kwa zaidi ya bilioni 83, kwa niaba ya wenzangu wa Dar es Salaam ninakushukuru mno,” amesema.

Pia amesema katika ujenzi wa barabara za mabasi yaendayo kasi wako kwenye hatua ya nne inaanzia Moroco mpaka Tegeta jumla kilometa 30.1 inayojengwa kwa zaidi ya bilioni 255.

Amesema kuna kipande cha Mwenge kilomita 4 kuja Ubungo ambacho ndicho kitatumika kwa kusaidiana na BRT 1 ambayo itawaleta wanunuzi na wafanyabiashara kwenye kituo kipya cha uwekezaji Ubungo.

Chalamila amesema maswali makubwa yamekuwa kama barabara zimeshakamilika kwa mfano barabara iendayo Mbagala imetengenezwa kwa kilomita 20.3 zaidi ya bilioni 217.

Aidha akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema idadi ya biashara katika Wilaya ya Ubungo zimeongezeka kutoka 4,220 mwaka 2020 mpaka kufikia 8,997 kwa mwaka 2025 ikiwa ni ongezeko la asilimia 113.

Amesema mradi huo utakuwa na jumla ya maduka 2,060 na mpaka wakati huu wa ufunguzi tayari kuna wafanyabiashara zaidi ya 400 waliopo hapo.

“Biashara Ubungo sasa zinaongezeka kwa kasi, mwaka 2020 tulikuwa na jumla la biashara 4,220 jimbo lote la Ubungo kwa sasa tuna biashara 8,997 ikiwa ni ongezeko la asilimia 113 ya biashara,” amesema na kuongeza;

“Maduka pekee mwaka 2020 yalikuwa 2,825 leo yapo 6,449 bila kuhesabu yanayoongezeka kupitia uwepo wa mradi huu maduka 2,060.”

Profesa Kitila amesema hiyo ina maana kuwa, ukiacha miradi inayoongezeka imefanya kuinua fursa za wananchi kimaisha na pia kukuza uchumi na hiyo ndiyo maana halisi ya kuinua nchi kiuchumi.

Amesema mradi huo ni wa nne kuzinduliwa kwa wiki hii, ukiwa ni miongoni mwa miradi muhimu ambayo ni sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji.

Akizungumzia maendeleo ya eneo hilo la Ubungo, Profesa Kitila amesema kuna maendeleo muhimu katika sekta mbalimbali zikiwemo za afya, elimu na maji.

Amesema mwaka 2020 Serikali iliahidi kuleta mradi wa barabara wa DMDP na katika jimbo la Ubungo limepata barabara 20 zenye urefu wa kilomita 25,000.

Amesema waliahidi barabara korofi iliyopo kata ya Kimara- Mavurunza – Bonyokwa mpaka Segerea inayopita katika majimbo matatu kujengwa tangu mwaka 2010 na haikuwahi kuingizwa katika bajeti, kutengewa fedha wala kupata mkandarasi.

“Mwaka 2023 iliingia katika bajeti na mwaka jana Desemba bilioni 3.6 ilitengwa na mkandarasi akaingia site kwa mara ya kwanza katika miaka 14 tangu iahidiwe, ni barabara ya kilomita 7 pekee lakini ni muhimu sana na imeleta faraja kubwa,” amesema.

Aidha Profesa Kitila amezungumzia changamoto waliyopata wananchi wenye makazi katika mito Gide na China ambao walipaza sauti kubomolewa nyumba zao suala lililoshughulikiwa kwa ujenzi wake kuingizwa katika mradi wa DMDP.