Dar es Salaam. Upatikanaji wa taulo za kike kwa ajili ya wanafunzi kujisitiri umepunguza tatizo la baadhi ya wasichana kukosa masomo kila mwezi wanapokuwa kwenye hedhi.
Wasichana hao hulazimika kubaki nyumbani wakihofia kuchafuka na kuaibika mbele za watu huku wakiwa hawana uwezo wa kupata tauli hizo kila mwezi.
Kwa mujibu wa utafiti uliotolewa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) mwaka 2023 unabainisha asilimia 60 ya wasichana wanashindwa kumudu gharama za ununuzi wa taulo za kike ambazo ni bidhaa muhimu katika maisha ya mtoto wa kike.

Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) katika sehemu yake ya kurudisha kwa jamii, imekabidhi taulo za kike 80,000 kwa wanafunzi wa shule mbalimbali za mkoa wa Geita katika jitihada za kuondoa changamoto hiyo.
Sambamba na hilo, walimu wa malezi wapatao 129 kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita walipatiwa mafunzo maalumu ya afya ya uzazi, ili kuwajengea uwezo wa kuwahudumia kwa ufanisi zaidi wanafunzi wa kike.
Lengo la jitihada hizo zikiwa ni kuongeza ufaulu wa wanafunzi hao na kupunguza utoro shuleni.
Akizungumza wakati wa hafla ya mafunzo hayo, Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Rehema Mustapha, amesema hatua hiyo imesaidia kupunguza utoro wa wanafunzi wa kike wakati wa hedhi na kuwafanya kuwa salama na kujiamini wakati wote.

“Zamani, kutokana na ugumu wa maisha, baadhi ya wanafunzi walikuwa hawafiki shuleni wakati wa hedhi na kukosa masomo, lakini tangu GGML iwe na utaratibu huu, hali imebadilika,” amesema.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyakabale, Veronica Samo, amesema hatua hiyo imeleta mabadiliko chanya kwa mahudhurio ya wanafunzi wa kike shuleni.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Mwalimu wa Malezi wa Shule ya Sekondari Nyakabale, Rosemary Nichoraus, kuwa msaada huo ni muarobaini wa changamoto waliokuwa wakikumbana nazo wasichana kipindi cha hedhi.
Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa GGML, Doreen Denis amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa kampuni hiyo wa kusaidia wasichana kubaki shuleni na kufikia ndoto zao.