Polisi waua watatu wanaodaiwa majambazi Kigoma

Kigoma/Mtwara. Watu watatu wanaodaiwa kuwa ni majambazi wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi mkoani Kigoma.

Watu hao wanaodaiwa kupanga kufanya unyang’anyi kwa kutumia silaha, wanadiwa kukutwa bunduki moja AK 47, magazine 1 ikiwa na risasi 10, bunduki iliyotengeneza kienyeji, visu viwili, panga  na marungu matatu.

Tukio hilo lilitokea usiku wa Julai 31, 2025 katika Kijji cha Kigendeka, Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma, ambapo askari waliokuwa katika doria walibaini njama za watu waliokuwa na lengo la kufanya unyang’anyi kwa kutumia silaha.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, Philemon Makungu, watu hao waliofunga barabara walidhibitiwa na polisi baada ya majibizano ya risasi yaliyosababisha vifo vya watu watatu.

“Kwenye majibizano hayo ya risasi, majambazi watatu ambao bado hawajatambuliwa kwa majina wala anuani za makazi, wameuawa baada ya kujeruhiwa na risasi, miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo kwa utambuzi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma linaendelea kuwaomba wananchi kufanya shughuli halali za kujingizia kipato zinazotambulika kwa mujibu wa sheria, tutaendelea kuchua hatua za kisheria kwa watu wote wanaojihusisha na uhalifu.

Tukio hilo la ujambazi linakuwa la tatu katika mwezi Julai baada ya lile la Julai 13, 2025 katika eneo la Kibaoni karibu na Kambi ya Wakimbizi Nduta.

Katika tukio hilo  watu waliodhaniwa kuwa majambazi waliweka vizuizi njiani katika Barabara ya Kaulu – Kibondo na kama fedha, simu, mabegi ya nguo na kompyuta mpakato, mali za abiria waliokuwa katika basi la Adventure likitokea Kigoma kwenda Mwanza na gari dogo aina ya Toyota Kluger.

Katika tukio jingine Julai 19, 2025 wavuvi waliokuwa wakiendelea na shughuli zao katika Ziwa Tanganyika walivamiwa na kundi la watu na kuwapora injini nne za boti aina ya Yamaha HP40.

Vingine vilivyoporwa katika tukio hilo ni  Betri 10 -N70, simu tano za mkononi  pamoja na mafuta ya dizeli lita 240 na taarifa iliyotolewa na Polisi ilithibitisha kushikiliwa kwa watu watatu kwa uchunguzi wa tukio hilo.

Katika hatua nyingine, jeshi hilo mkoani Mtwara limekanusha taarifa zilizochapishwa na msanii Anastazi Mahatane maarufu kama Ebitoke kuwa maisha yake yapo hatarini kwa kuwa kuna watu wanataka kumuua.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram Julai 30, 2025 Ebitoke ambaye kwa sasa anaishi Mtwara alichapisha taarifa akieleza ametumbukizwa katika shimo katika fukwe za Msanga Mkuu na kwamba wapo watu ambao aliwataja kwa majina kuwa wanataka kumuua.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman amesema baada ya kupata taarifa hizo uchunguzi wa haraka uliohusisha kumtafuta na kumkamata Ebitoke aliyekutwa kwenye ufukwe wa Msanga Mkuu akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa.

“Katika uchunguzi wa awali, Jeshi la Polisi limebaini Ebitoke alifika mkoani Mtwara tangu Aprili 2025 na kufikia katika hoteli moja iliyopo Msanga Mkuu na kuomba hifadhi kwa watu waliokuwa wanafahamiana kabla ya maisha yake kumwendea vibaya huko alikokuwa.

“Alikamatwa Julai 31, 2025 saa 11:00 jioni katika fukwe za Msanga Mkuu akiwa katika hali inayoonekana kuwa amechanganyikiwa na hakuwa ametumbukizwa katika shimo wala kutekwa kama ambavyo alivyokuwa ameeleza katika mitandao hiyo ya kijamii.”

Taarifa hiyo inaeleza kuwa kwa sasa Ebitoke yupo katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara kwa ajili ya matibabu, hivyo ndugu na jamaa zake wametakiwa kufika Mtwara kutoa msaada au kumchukua ndugu yao.