Ibenge: Wiki mbili tu zinatosha

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge amesema wiki mbili jijini Arusha zitatosha kutoa uelekeo wa maandalizi ya msimu mpya, huku akiweka wazi ameona mwanga baada ya kukuutana na wachezaji  na kuzungumza na mmoja mmoja.

Azam kabla ya kuondoka jijini mapema leo kwenda Arachuga, walikuwa na siku tatu za maandalizi ambapo kocha alipata nafasi ya kuzungumza na nyota ambao hawajapata nafasi ya kuziotumikia timu zao za taifa kwenye michuano ya CHAN sambamba na nyota wapya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ibenge alisema anamatarajio makubwa baada ya kuzungumza na mchezaji mmoja mmoja na kubaini kila mmoja malengo ni sawa na ya klabu hivyo mikakati aliyonayo sasa ni kuandaa jeshi imara la ushindani ambalo litampa matokeo mazuri.

“Ni mapema sana kuzungumza juu ya maandalizi kwa sababu ndiyo kwanza nimekuwa na siku tatu za kukaa na wachezaji wangu na leo (jana) tumeanza safari ya kwenda Arusha na tutakuwa na wiki mbili za maandalizi,” alisema Ibenge na kuongeza;

“Naamini huko ndio nitakuwa na kazi ya kufanya kuhakikisha naandaa kikosi licha ya baadhi ya wachezaji kutokuwa pamoja na mimi lakini naamini waliopo watanipa picha zaidi ya aina ya kikosi nilichonacho na malengo ya msimu nipo Tanzania nchi ambayo ina ushindani mkubwa kisoka.”

Kikosi cha Azam kikiwa Karatu kitakuwa na wiki mbili kuanzia Agosti 1 hadi 14 na itacheza mechi za kirafiki ambazo zitawapa kipimo sahihi cha maandalizi waliyoyafanya.

Inaelezwa timu hiyo bado haijakamilisha usajili na itatumia michuano ya CHAN kutafuta nyota wengine ili kuwa na kikosi bora na cha ushindani masimu ujao malengo ni kufanya vizuri ndani na kimataifa wakiwa wawakilishi Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.