Beki Simba abariki usajili wa Sowah

BAADA ya kuitumikia Simba kwa misimu miwili na kutimkia USM Alger ya Algeria, beki Fondoh Che Malone ameupongeza uongozi wa timu hiyo kunasa saini ya Jonathan Sowah aliyemtaja ni miongoni mwa washambuliaji bora aliowahi kukutana nao.

Che Malone aliyesajiliwa misimu miwili iliyopita kutoka Cotonsport ya Cameroon, amemtaja pia kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids ni zaidi ya kocha kwake, kwani licha ya changamoto nyingi dhidi yake alimwamini na kumpa nafasi akimjenga kuwa mchezaji bora anayeweza akafanya makubwa.

Beki huyo amejiunga na USM Alger baada ya Simba kufanya biashara na timu hiyo na tayari ametambulishwa na kuanza maandalizi ya msimu mpya.

Akizungumza na Mwanaspoti, Che Malone alisema kwa nafasi yake amekutana na wachezaji wengi wazuri na bora bila kujali ni wazawa au wageni hawezi kumtaja mmoja mmoja lakini kwa Sowah ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa ataisaidia Simba msimu ujao na atafanya vizuri eneo hilo.

“Nimekutana na washambuliaji wengi wazuri wa kitanzania na wa kigeni kwa kuwa umemzungumzia Sowah na kunihakikishia anaenda Simba basi naomba kumtolea ufafanuzi huyo naamini benchi la ufundi na uongozi wa timu umefanya uamuzi sahihi kumsajili atawasaidia,” alisema Che Malone na kuongeza;

“Sowah ni mshambuliaji aliye kamilika, sio wa kusubiri ndani ya 18 ana uwezo wa kushambulia na kukaba, anatafuta na anaweza kukaa kwenye nafasi na ana kasi, nguvu na juhudi naamini atafanya makubwa ni mingoni mwa washambuliaji bora msimu ulioisha namfananisha na Fiston Mayele.”

Akizungumzia maisha yake Simba, alisema alikuwa na misimu miwili migumu na bora licha ya changamoto zote ameondoka akiwa amejifunza mambo mengi ambayo yamemjengea kujiamini na kudai safari moja huanzisha nyingine.

“Napenda kusema asante kwa wachezaji wenzangu, benchi zima la ufundi, madaktari na uongozi wote wa Simba kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kucheza timu hiyo yenye historia kubwa, nakiri nilikuwa na misimu miwili bora licha ya changamoto za hapa na pale sijafanikiwa kuipa taji lolote lakini kucheza fainali ni sehemu ya mafanikio makubwa niliyoyapata,” alisema Che Malone na kuongeza;

“Ningependa kuendelea na safari na timu hiyo lakini unajua soka huja na fursa nyingine nimeamua kuondoka kupata changamoto nyingine. Shukrani za pekee ziende pia kwa mashabiki ambao waliniunga mkono bila kuchoka katika nyakati nzuri na mbaya ni sehemu ya watu ambao wapo kwaajili ya ukosoaji, kutia moyo, msukumo asanteni kwa upendo mlionionyesha.”