Msimamo wa wajumbe Kigamboni, Ilala kuwapata mbunge sahihi

Dar es Salaam. Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Wilaya ya Kigamboni na Ilala, wamesema watatumia turufu ya kura zao kutoa nafasi kwa mtiania mmoja wa ubunge na wa udiwani kwa kuzingatia uwezo wa kutatua changamoto zao.

Mbali na hilo, wameapa kutohadaika na kauli na maneno matamu ya wagombea, kwa kuwa wengi wao kujenga ushawishi huo ili wapitishwe katika kura za maoni, kisha baadaye wanakata mawasiliano.

Kwa upande wa wajumbe wa Kigamboni, wamesema eneo hilo linakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo tozo kwenye Daraja la Mwalimu Nyerere, vivuko vya Magogoni-Kigamboni, kuvamiwa kwa maeneo ya wazi na kujengwa vituo vya mafuta, ajira kwa vijana na kulinda mapato ya manispaa.

Wakati Ilala, wamesema hali iliyonayo jimbo hilo ni tofauti na uhalisia wa lilivyopaswa kuwa, iwapo fursa zilizopo zingetumiwa vema na wakazi.

Hayo yamejiri leo, Ijumaa Agosti 1, 2025 katika ziara za watiania wa ubunge na udiwani walipokwenda kujitambulisha katika majimbo hayo, kuelekea kura za maoni Agosti 4, mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi, Marco Macha ambaye ni Mjumbe kutokea Kata ya Tungi, amesema wanahitaji muwakilishi jasiri atakayekuwa mstari wa mbele kupigania maslahi ya wananchi.

“Umeona Kigamboni uwekezaji kila sehemu za wazi zitachukuliwa na wawekezaji hatuna sehemu ambazo hata vijana wetu wanaweza kusema wakacheze mpira, hukuna sehemu ya kwenda kupunga upepo ukichoka.

“Wanajenga vituo vya mafuta kila kona hakuna kiongozi anayefikiria ikiwa ajali ya moto Usalama wetu utakuwaje, tunataka mbunge atakayekuja kuweka ukomo,” amesema Macha.

Kwa upande wake Evalister Mbando, mjumbe kutoka Vijibweni amesema wanahitaji mtu atakayeenda bungeni kupaza sauti walitumie daraja la Nyerere bila kutozwa tozo kama ilivyo katika Daraja la Tanzanite na mengine.

“Wenzetu hawatozwi chochote kwani Kigamboni tunaishi watu gani, tunatamani Serikali iondoe jambo hili, bado hatujapata ufumbuzi magari, bajaji na pikipiki zinatozwa utafikiri unaingia nchi zingine,” amesema Mbando.

Ilipofikia hatua ya watiania sita kujinadi, kila mmoja alikuwa anajenga hoja kuwashawishi wajumbe ikiwa atachaguliwa atafanyaje ili kuwa mwakilishi bora.

“Niwakati wa wananchi wa Kigamboni kuamua kupata kiongozi bora au muwakili, binafsi nastahili kuliko wengine wote kwakuwa nazijua shida za wananchi wa Kigamboni kwakuwa tangu mdogo naishi huku najua kuna shida ya ardhi nichague nikawe muwakilishi bora,” Mchange Mchange mgombea.

Cynthia Henjewele, amesema iwapo atapewa nafasi atakubali kuwa mtumwa wa wananchi kwa kusemea changamoto zao ili hatua zichukuliwe na Serikali.

“Kigamboni changamoto tunazo nyingi pamoja na kwa Serikali inajitahidi kuzitatua lakini nahitaji kura zenu ili niende bungeni nikaendeleze tulipoishia,” amesema.

Wagombea wengine wa Ubunge Kigamboni ni Mponela Matei, Haran Sanga, Ally Mandai na Francis Mwakitalu.

Kwa upande wa Ilala, wakiwa katika Kata ya Mchikichini, mmoja wa wajumbe Hakidhi Waziri, amehoji changamoto zipi zinazowasumbua wakazi wa jimbo hilo.

“Changamoto ni nyingi kubwa ikiwemo tatizo la ajira kwani pamoja na Ilala kuzungukwa na fursa nyingi ikiwemo soko la Karume bado hatujalitumia vilivyo na zaidi wanaofaidika ni kutoka maeneo mengine,” amesema Joseph Ngoa mmoja wa watiania.

Nurdin Bilal maarufu Shetta anayewania udiwani wa Mchikichini, amesema kutokana na kumiliki taasisi ya Sawa inayoshughulika na uwezeshaji wa wasichana na kina mama, ataitumia kutoa elimu kwa vijana kujikwamua kiuchumi na kuwawezesha kutumia fursa zilizopo.

Kwa upande wa Milard Mpangala mtiania wa ubunge, amesema kipaumbele chake ni siasa safi na uchumi.

Kuhusu uchumi, amesema anaona Ilala imezungukwa na fursa nyingi lakini imeshindikana kuzitumia, hivyo akipewa nafasi atalifanikisha hilo.

Kwa upande wa Mussa Zungu anayetetea nafasi yake, amesema inasikitisha hata kwenye mikopo ya halmashauri watu wamekuwa wakiogopa kwenda kuichukua kwa sababu ya utaratibu, hivyo wanapaswa kujitokeza kwenda kuomba.

Stella Njau amesema ameamua kuchukua uamuzi huo wa kuutaka ubunge kwa sababu ni kijana, ana uwezo na ana nguvu ya kuwatumikia wananchi.