WAKATI tetesi mbalimbali zikidai winga wa Simba, Ellie Mpanzu anaweza kuondoka dirisha hili, taarifa kutoka chanzo cha kuaminika Simba zimesema mchezaji huyo bado yupo sana na kesho Jumapili atatua baada ya awali kuomba udhuru kumaliza mambo akiwa kwao DR Congo.
Mara baada ya kutua, mchezaji huyo ataungana na wachezaji wengine wakiwamo wapya, Jonathan Sowah kupaa kuwahi kambi ya timu hiyo kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya iliyopo Ismailia, Misri.
Akizungumza na Mwanaspoti, kiongozi mmoja wa Simba (jina tunalo, alisema wachezaji wote ambao wamechelewa kuingia kambini ni kwa sababu ya masuala ya viza.
“Inashangaza kuona Mpanzu anahusishwa na timu nyingine wakati ana mkataba wa miaka miwili na Simba na endapo kama angekuwa anauzwa basi tungetangaza kama ilivyo kwa wengine waliyouzwa ili kuwa na taarifa sahihi kwa jamii, lakini tumeamua kunyamaza ili waje wamuone uwanjani,” alisema kiongozi huyo na kuongeza;
“Wachezaji waliyopo kambini Misri tulikuwa nao msimu uliyopita ambao katika mfumo wa viza ilikuwa rahisi kukamilisha kwa uharaka na ikumbukwe tumewasajili kutoka nchi mbalimbali, lazima wafike Dar es Salaam washughulikie viza kisha waanze safari ya kwenda kambini kujiunga na wenzao.
“Mfano Kibu Denis aliingia Dar es Salaam Jumatano na juzi (jana) Alhamisi alianza safari ya kwenda Misri kujiunga na wenzao, kipa Moussa Camara aliingia kambini Jumatano Alhamisi alifanya mazoezi na wenzake.
“Simba inaendelea na usajili, usishangae wachezaji kuingia kwa mafungu kambini, kulingana na mchakato utakaofanyika wa utaratibu unaotakiwa, hivyo kikosi kinaweza kikakamilika hadi kufikia Jumapili, kikubwa mashabiki watulie waamini kile ambacho kinafanywa na uongozi wao.”